Lk. 8:32-52 Swahili Union Version (SUV)

32. Basi, hapo palikuwa na kundi la nguruwe wengi wakilisha mlimani; wakamsihi awape ruhusa kuwaingia wale. Akawapa ruhusa.

33. Pepo wakamtoka mtu yule wakawaingia nguruwe, nalo kundi lilitelemka gengeni kwa kasi, wakaingia ziwani, wakafa maji.

34. Wachungaji walipoona lililotokea walikimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani.

35. Watu wakatoka kwenda kuliona lililotokea, wakamwendea Yesu, wakamwona mtu yule aliyetokwa na pepo ameketi miguuni pa Yesu, amevaa nguo, ana akili zake; wakaogopa.

36. Na wale waliokuwa wameona waliwaeleza jinsi alivyoponywa yule aliyepagawa na pepo.

37. Na jamii ya watu wa nchi ya Wagerasi iliyo kando kando walimwomba aondoke kwao, kwa kuwa walishikwa na hofu nyingi; basi akapanda chomboni, akarudi.

38. Na mtu yule aliyetokwa na pepo alimwomba ruhusa afuatane naye; lakini yeye alimwaga akisema,

39. Rudi nyumbani kwako, ukahubiri yalivyo makuu Mungu aliyokutendea. Akaenda zake, akihubiri katika mji wote, yalivyo makuu mambo aliyotendewa na Yesu.

40. Basi Yesu aliporudi mkutano ulimkaribisha kwa furaha, maana walikuwa wakimngojea wote.

41. Na tazama, mtu mmoja akaja, jina lake Yairo, naye ni mtu mkuu wa sinagogi, akaanguka miguuni pa Yesu, akamsihi aingie nyumbani kwake;

42. kwa kuwa binti yake yu katika kufa, ambaye ni mwana pekee, umri wake amepata miaka kumi na miwili. Na alipokuwa akienda makutano walimsonga.

43. Na mwanamke mmoja, ambaye ametokwa na damu muda wa miaka kumi na miwili, [aliyekuwa amegharimiwa mali zake zote kwa kuwapa waganga] asipate kuponywa na mtu ye yote,

44. alikwenda nyuma yake, akaugusa upindo wa vazi lake; na mara hiyo kutoka damu kwake kulikoma.

45. Yesu akasema, Ni nani aliyenigusa? Basi, watu wote walipokana, Petro alimwambia, Bwana mkubwa, makutano haya wanakuzunguka na kukusonga.

46. Yesu akasema, Mtu alinigusa, maana naona ya kuwa nguvu zimenitoka.

47. Yule mwanamke, alipoona ya kwamba hawezi kusitirika akaja akitetemeka, akaanguka mbele yake, akamweleza mbele ya watu wote sababu yake ya kumgusa, na jinsi alivyoponywa mara.

48. Akamwambia Binti, imani yako imekuponya; enenda zako na amani.

49. Alipokuwa akinena hayo, alikuja mtu kutoka nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akamwambia, Binti yako amekwisha kufa; usimsumbue mwalimu.

50. Lakini Yesu aliposikia hayo, alimjibu, Usiwe na hofu, amini tu, naye ataponywa.

51. Alipofika nyumbani hakuacha mtu kuingia pamoja naye ila Petro, na Yohana, na Yakobo, na babaye yule mtoto na mamaye.

52. Na watu wote walikuwa wakilia na kumwombolezea; akasema, Msilie, hakufa huyu, bali amelala usingizi tu.

Lk. 8