5. Usimchinje pasaka ndani ya malango yako yote akupayo BWANA, Mungu wako;
6. ila mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako, apakalishe jina lake, ndipo mtakapomchinja pasaka jioni, katika machweo ya jua, kwa wakati kama uliotoka Misri.
7. Nawe umwoke na kumla mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako; kisha asubuhi yake ugeuke uende hemani mwako.
8. Siku sita utakula mikate isiyotiwa chachu; na siku ya saba na uwe mkutano mtukufu kwa BWANA, Mungu wako, usifanye kazi yo yote.
9. Jihesabie majuma saba; tangu wakati uanzao kutia mundu katika mmea utaanza kuhesabu majuma saba.
10. Nawe sikukuu ya majuma umfanyie BWANA, Mungu wako, kwa kutoa sadaka ya hiari ya mkono wako, utakayotoa kwa kadiri akubarikiavyo BWANA, Mungu wako;
11. nawe utafurahi mbele ya BWANA, Mungu wako, wewe na mwana wako na binti yako, na mtumwa wako na mjakazi wako, na Mlawi aliye ndani ya malango yako, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio katikati yako, katika mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako, apakalishe jina lake.
12. Nawe kumbuka kwamba ulikuwa mtumwa huko Misri; tena zishike amri hizi kwa kuzifanya.
13. Fanya sikukuu ya vibanda siku saba, utakapokwisha kuyakusanya yatokayo katika sakafu yako ya nafaka, na katika kinu chako cha divai;
14. nawe utafurahi katika sikukuu yako, wewe, na mwanao, na binti yako, na mtumwa wako, na mjakazi wako, na Mlawi, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio ndani ya malango yako.
15. Siku saba mfanyie sikukuu BWANA, Mungu wako, mahali atakapochagua BWANA; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, atakubarikia katika maongeo yako yote, na katika kazi zote za mikono yako, nawe uwe katika kufurahi kabisa.
16. Mara tatu kwa mwaka na watokee wanawaume wako wote mbele za BWANA, Mungu wako, mahali atakapochagua; katika sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, na katika sikukuu ya majuma, na katika sikukuu ya vibanda; wala wasitokee mbele za BWANA mikono mitupu.
17. Kila mtu na atoe kama awezavyo, kwa kadiri ya baraka ya BWANA, Mungu wako, alivyokupa.
18. Weka waamuzi na maakida katika malango yako yote akupayo BWANA, Mungu wako, kwa hesabu ya kabila zako; nao wawaamue watu kwa maamuzi ya haki.
19. Usipotoe maamuzi; wala usipendelee uso wa mtu; wala usitwae rushwa; kwa kuwa rushwa hupofusha macho ya wenye akili, na kugeuza daawa ya wenye haki.
20. Yaliyo haki kabisa ndiyo utakayoyafuata, ili upate kuishi na kuirithi nchi upewayo na BWANA, Mungu wako.
21. Usipande mti uwao wote kuwa Ashera kwako kando ya madhabahu utakayofanya ya BWANA, Mungu wako.