Kum. 15:6-18 Swahili Union Version (SUV)

6. Kwani BWANA, Mungu wako, atakubarikia, kama alivyokuahidi; nawe utakopesha mataifa mengi, lakini hutakopa; tena utayatawala mataifa mengi, usitawaliwe na wao.

7. Kama akiwapo mtu maskini pamoja nawe, nduguzo mmojawapo, ndani ya malango yako mojawapo, katika nchi yako akupayo BWANA, Mungu wako, usifanye moyo wako kuwa mgumu, wala usimfumbie mkono wako nduguyo maskini;

8. lakini mfumbulie mkono wako kwa kweli, umkopeshe kwa kweli yatoshayo haja yake katika ahitajiayo.

9. Jitunze, msiwe na neno lisilofaa moyoni mwako, kusema, Umekaribia mwaka wa saba, mwaka wa maachilio; jicho lako likawa ovu juu ya nduguyo usimpe kitu; naye akamlilia BWANA juu yako, ikawa ni dhambi kwako.

10. Mpe kwa kweli, wala moyo wako usisikitike utakapompa; kwa kuwa atakubarikia BWANA, Mungu wako, kwa neno hili katika kazi yako yote, na katika kila utakalotia mkono wako.

11. Kwa maana maskini hawatakoma katika nchi milele; ndipo ninakuamuru na kukuambia, Mfumbulie kwa kweli mkono wako nduguyo, mhitaji wako, maskini wako, katika nchi yako.

12. Ikiwa nduguyo, mume wa Kiebrania, au mwanamke wa Kiebrania, akiuzwa kwako, naye amekutumikia miaka sita; basi mwaka wa saba mwache huru aondoke kwako.

13. Nawe utakapomwacha huru aondoke kwako, usimwache aende zake mikono mitupu;

14. umwangalie kwa wema katika kundi lako, na sakafu yako ya nafaka, na kinu chako cha divai; mpe kama alivyokubarikia BWANA, Mungu wako.

15. Nawe kumbuka kwamba ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, akakukomboa BWANA, Mungu wako; kwa hiyo mimi nakuamuru neno hili hivi leo.

16. Hata itakuwa, akikuambia, Siondoki kwako; kwa sababu akupenda wewe na nyumba yako, kwa kuwa yu hali njema kwako;

17. ndipo utwae uma, uupenyeze katika sikio lake uingie katika ubao wa mlango, naye atakuwa mtumishi wako milele. Na kijakazi chako naye mfanye vivyo.

18. Wala usione ugumu, utakapomwacha huru kuondoka kwako; kwani amekutumikia miaka sita kwa ujira mara mbili wa mwajiriwa; na BWANA, Mungu wako, atakubarikia kwa yote utakayofanya.

Kum. 15