1. Ikawa mfalme Hezekia aliposikia hayo, alizirarua nguo zake, akajivika nguo za magunia, akaingia katika nyumba ya BWANA.
2. Akamtuma Eliakimu aliyekuwa msimamizi wa nyumba yake na Shebna, mwandishi, na wazee wa makuhani, wamejivika nguo za magunia, waende kwa Isaya nabii, mwana wa Amozi.
3. Wakamwambia, Hezekia asema hivi, Siku hii ni siku ya dhiki, na aibu, na matukano; maana watoto wa tayari kuzaliwa, wala hapana nguvu za kuwazaa.
4. Yamkini BWANA, Mungu wako, atayasikia maneno ya huyo amiri ambaye mfalme wa Ashuru, bwana wake, amemtuma ili amtukane Mungu aliye hai; na BWANA, Mungu wako atayakemea maneno aliyoyasikia; basi, inua dua yako kwa ajili ya mabaki yaliyobakia.
5. Basi, watumishi wa mfalme Hezekia wakaenda kwa Isaya.
6. Isaya akawaambia, Mwambieni bwana wenu maneno haya; BWANA asema hivi, Usiyaogope maneno uliyoyasikia, ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wamenitukana.
7. Tazama, nitatia roho ndani yake, naye atasikia kivumi, na kurudi hata nchi yake mwenyewe, nami nitamwangusha kwa upanga katika nchi yake mwenyewe.
8. Basi yule amiri akarudi, akamkuta mfalme wa Ashuru anafanya vita juu ya Libna; kwa maana alikuwa amesikia ya kwamba ameondoka, akaacha Lakishi.
9. Naye alisikia habari ya Tirhaka, mfalme wa Kushi, ya kwamba, Ametoka ili kupigana nawe; naye aliposikia hayo, akatuma wajumbe kwa Hezekia, kusema,
10. Mwambieni Hezekia, mfalme wa Yuda, maneno haya, mkisema, Asikudanganye Mungu wako unayemtumaini, akisema, Yerusalemu hautatiwa katika mikono ya mfalme wa Ashuru.
11. Tazama, umesikia habari ya mambo yote, ambayo wafalme wa Ashuru wamezitenda nchi zote, kwa kuziangamiza kabisa je! Utaokoka wewe?