Isa. 2:5-18 Swahili Union Version (SUV)

5. Enyi wa nyumba ya Israeli, njoni, twende katika nuru ya BWANA.

6. Maana wewe umewaacha watu wako, nyumba ya Israeli, kwa sababu wamejaa kawaida za mashariki, nao ni wapiga ramli kama Wafilisti, na wanapana mikono na wana wa wageni.

7. Tena nchi yao imejaa fedha na dhahabu, wala hapana mwisho wa hazina zao; tena nchi yao imejaa farasi, wala hapana mwisho wa magari yao.

8. Tena nchi yao imejaa sanamu; huabudu kazi ya mikono yao, vitu vilivyofanywa kwa vidole vyao wenyewe.

9. Mtu mnyonge huinama, na mtu mkubwa hujidhili; kwa hiyo usiwasamehe.

10. Ingia ndani ya jabali; ukajifiche mavumbini mbele za utisho wa BWANA, mbele za utukufu wa enzi yake.

11. Macho ya mwanadamu yaliyoinuka yatashushwa chini, na kiburi cha mwanadamu kitainamishwa, naye BWANA, yeye peke yake, atatukuzwa siku hiyo.

12. Kwa maana kutakuwa siku ya BWANA wa majeshi juu ya watu wote wenye kiburi na majivuno, na juu ya yote yaliyoinuka; nayo yatashushwa chini.

13. Na juu ya mierezi yote ya Lebanoni iliyo mirefu na kuinuka, na juu ya mialoni yote ya Bashani;

14. na juu ya milima mirefu yote, na juu ya vilima vyote vilivyoinuka;

15. na juu ya kila mnara mrefu, na juu ya kila ukuta ulio na boma;

16. na juu ya merikebu zote za Tarshishi, na juu ya kila taswira ipendezayo.

17. Na majivuno ya mwanadamu yatainamishwa, na kiburi cha watu kitashushwa; naye BWANA, yeye peke yake, atatukuzwa siku hiyo.

18. Nazo sanamu zitatoweka kabisa.

Isa. 2