15. Wala haitakuwako kazi yo yote katika Misri iwezayo kufanywa, ya kichwa au ya mkia, ya tawi au ya nyasi.
16. Katika siku hiyo Misri itakuwa kama wanawake; itatetemeka na kuogopa kwa sababu ya kutikiswa kwa mkono wa BWANA wa majeshi, autikisao juu yake.
17. Na nchi ya Yuda itakuwa sababu ya utisho kwa Misri; kila mtu atakayeambiwa habari zake ataingiwa na woga, kwa sababu ya kusudi la BWANA wa majeshi, analolikusudia juu yake.
18. Katika siku hiyo itakuwako miji mitano katika nchi ya Misri itumiayo lugha ya Kanaani, na kumwapia BWANA wa majeshi; mji mmoja utaitwa Mji wa uharibifu.
19. Katika siku hiyo itakuwako madhabahu katika nchi ya Misri kwa BWANA, na nguzo mpakani mwake kwa BWANA.
20. Nayo itakuwa ishara na ushuhuda kwa BWANA wa majeshi katika nchi ya Misri; kwa maana watamlilia BWANA kwa sababu ya watu wawaoneao, naye atawapelekea mwokozi mwenye kuwatetea, naye atawaokoa.
21. Na BWANA atajulikana na Misri, na Wamisri watamjua BWANA katika siku hiyo; naam watamtumikia kwa dhabihu na matoleo, nao watamwekea BWANA nadhiri, na kuzitekeleza.
22. Naye BWANA atapiga Misri, akipiga na kuponya; nao wakirudi kwa BWANA, atakubali maombi yao na kuwaponya.
23. Katika siku hiyo itakuwako njia kuu itokayo Misri na kufika hata Ashuru; Mwashuri atafika Misri, na Mmisri atafika Ashuru, na Wamisri wataabudu pamoja na Waashuri.
24. Katika siku hiyo Israeli atakuwa wa tatu pamoja na Misri na Ashuru, watakuwa baraka kati ya dunia;
25. kwa kuwa BWANA wa majeshi amewabariki, akisema, Wabarikiwe watu wangu Misri; na wewe Ashuru, kazi ya mikono yangu; na wewe Israeli, urithi wangu.