1. Na mambo hayo yalipokwisha kutendeka, wakuu wakanikaribia, wakisema, Watu wa Israeli, na makuhani, na Walawi, hawakujitenga na watu wa nchi hizi, wamefanya sawasawa na machukizo yao, yaani, ya Wakanaani, na Wahiti, na Waperizi, na Wayebusi, na Waamoni, na Wamoabi, na Wamisri, na Waamori.
2. Maana wametwaa binti zao kuwa wake zao, na wake za watoto wao; basi mbegu takatifu wamejichanganya na watu wa nchi hizi; naam, mkono wa wakuu na mashehe umetangulia katika kosa hili.
3. Nami niliposikia hayo, nikararua nguo yangu na joho yangu, nikang’oa nywele za kichwa changu, na ndevu zangu, nikaketi kwa mshangao.
4. Ndipo wakanikusanyikia watu wote walioyatetemekea maneno ya Mungu wa Israeli, kwa sababu ya lile kosa la watu wa uhamisho; nami nikaketi kwa mshangao hata wakati wa sadaka ya jioni.
5. Na wakati wa sadaka ya jioni nikainuka baada ya kunyenyekea kwangu, nguo yangu na joho yangu zimeraruliwa, nikaanguka magotini nikakunjua mikono yangu mbele za BWANA, Mungu wangu;
6. nikasema, Ee Mungu wangu, nimetahayari, naona haya kuinua uso wangu mbele zako, Mungu wangu; kwa maana maovu yetu ni mengi, hata yamefika juu ya vichwa vyetu, na hatia yetu imeongezeka na kufika mbinguni.
7. Tangu siku za baba zetu tumekuwa na hatia kupita kiasi hata leo; na kwa sababu ya maovu yetu sisi, na wafalme wetu, na makuhani wetu, tumetiwa katika mikono ya wafalme wa nchi hizi, tumepigwa kwa upanga, tumechukuliwa mateka, tumenyang’anywa mali zetu, tumetiwa haya nyuso zetu, kama hivi leo.
8. Na sasa kwa muda kidogo tumeneemeshwa na BWANA, Mungu wetu, hata akatuachia mabaki yaokoke, akatupa msumari katika mahali pake patakatifu. Mungu wetu atutie nuru machoni mwetu, tuburudike kidogo katika kufungwa kwetu.
9. Maana sisi tu watumwa; lakini Mungu wetu hakutuacha katika utumwa wetu, bali ametufikilizia rehema zake, mbele ya wafalme wa Uajemi, ili kutuburudisha, kuisimamisha nyumba ya Mungu wetu, na kuitengeneza palipobomoka, atupe ukuta katika Yuda na Yerusalemu.