1. Ikawa katika mwaka wa kumi na mmoja, mwezi wa tatu, siku ya kwanza ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema,
2. Mwanadamu, mwambie Farao mfalme wa Misri, na jamii ya watu wake, Je! Umefanana na nani katika ukuu wako?
3. Tazama, Mwashuri alikuwa mwerezi katika Lebanoni, wenye matawi mazuri, na kifuniko chenye uvuli, na kimo kirefu; na kilele chake kilikuwa kati ya matawi mapana.
4. Maji yalimlisha, vilindi vilimsitawisha; mito yake ilipita pande zote za miche yake; naye akapeleka mifereji yake kwa miti yote ya kondeni.
5. Basi kimo chake kilitukuzwa kuliko miti yote ya kondeni, na vitanzu vyake viliongezeka; matawi yake yakawa marefu, kwa sababu ya maji mengi, alipoyachipuza.
6. Ndege wote wa angani walifanya vioto vyao katika vitanzu vyake, na chini ya matawi yake wanyama wote wa kondeni walizaa watoto wao, na chini ya uvuli wake mataifa makuu yote walikaa.