2 Sam. 19:7-24 Swahili Union Version (SUV)

7. Basi sasa, ondoka, utoke nje, ukaseme na watumishi wako maneno ya kuwatuliza roho zao; maana mimi nakuapia kwa BWANA, usipotoka, hatabaki hata mtu mmoja pamoja nawe usiku huu; na mambo haya yatakuwa mabaya kwako kuliko mabaya yote yaliyokupata tokea ujana wako hata sasa.

8. Ndipo mfalme akaondoka, akaketi langoni. Nao wote wakaambiwa ya kwamba, Angalieni, mfalme ameketi langoni; watu wote wakaenda huko mbele ya mfalme.Basi, Israeli wote walikuwa wamekimbia kila mtu hemani kwake.

9. Wakashindana watu wote katika kabila zote za Israeli, wakisema, Mfalme alitutoa mikononi mwa adui zetu, akatuokoa mikononi mwa Wafilisti; naye sasa amekimbia kutoka nchi hii mbele ya Absalomu.

10. Na huyo Absalomu, tuliyemtia mafuta ili awe juu yetu, amekufa vitani. Basi sasa mbona ninyi hamsemi neno lo lote juu ya kumrudisha tena mfalme?

11. Naye mfalme Daudi akatuma kwa Sadoki na Abiathari, makuhani, kusema, Neneni na wazee wa Yuda, mkisema, Kwa nini ninyi mmekuwa wa mwisho wa kumrudisha tena mfalme nyumbani kwake? Kwa maana maneno ya Israeli wote yamemjia mfalme, ili kumleta nyumbani kwake.

12. Ninyi ni ndugu zangu, ninyi ni mfupa wangu na nyama yangu; mbona basi ninyi mmekuwa wa mwisho wa kumrudisha tena mfalme.

13. Kisha mkamwambie Amasa, Je! Si wewe uliye mfupa wangu, na nyama yangu? Mungu anifanyie hivyo, na kuzidi, usipokuwa wewe jemadari wa jeshi mbele yangu daima mahali pa Yoabu.

14. Akawainamisha mioyo watu wote wa Yuda, kama mtu mmoja; basi wakatuma kwa mfalme, Rudi wewe na watumishi wako wote.

15. Hivyo mfalme akarudi, akafika Yordani. Kisha Yuda wakaja Gilgali kwenda kumlaki mfalme, na kumvusha mfalme Yordani.

16. Akafanya haraka Shimei, mwana wa Gera, Mbenyamini, wa Bahurimu akashuka pamoja na watu wa Yuda ili kumlaki mfalme Daudi.

17. Na Watu elfu wa Benyamini walikuwa pamoja naye, na huyo Siba mtumwa, nyumba ya Sauli, na hao wanawe kumi na watano, na watumwa wake ishirini pamoja naye; wakavuka Yordani mbele ya mfalme.

18. Tena ikavuka mashua ili kuwavusha jamaa ya mfalme, na kufanya aliyoyaona kuwa mema.Ndipo Shimei, mwana wa Gera, akamwangukia mfalme alipokuwa amevuka Yordani.

19. Akamwambia mfalme, Bwana wangu asinihesabie uovu, wala usiyakumbuke yale niliyoyatenda mimi mtumwa wako kwa upotoe siku ile alipotoka Yerusalemu bwana wangu mfalme, hata mfalme ayatie moyoni mwake.

20. Kwa kuwa mimi mtumwa wako najua ya kwamba nimekosa; kwa hiyo, tazama, nimekuja leo, wa kwanza wa nyumba yote ya Yusufu, kushuka ili nimlaki bwana wangu mfalme.

21. Lakini Abishai, mwana wa Seruya, akajibu na kusema, Je! Shimei hatauawa kwa sababu hii, kwa kuwa amemlaani masihi wa BWANA?

22. Lakini Daudi akasema, Mimi nina nini nanyi, enyi wana wa Seruya, hata mmekuwa adui zangu leo? Je! Atauawa mtu ye yote leo katika Israeli? Kwa maana sijui mimi leo ya kwamba ndimi mfalme juu ya Israeli?

23. Kisha mfalme akamwambia Shimei, Hutakufa. Mfalme akamwapia.

24. Kisha Mefiboshethi, mwana wa Sauli, akashuka ili amlaki mfalme; alikuwa hakukata kucha za miguu yake wala kukata ndevu zake, wala kufua nguo zake, tangu siku alipoondoka mfalme, hata siku hiyo aliporudi kwake kwa amani.

2 Sam. 19