2. Daudi akawapeleka hao watu vitani, theluthi moja chini ya mkono wa Yoabu, na theluthi ya pili chini ya mkono wa Abishai, mwana wa Seruya nduguye Yoabu, na theluthi ya tatu chini ya mkono wa Itai, Mgiti. Mfalme akawaambia watu, Bila shaka mimi mwenyewe nami nitatoka pamoja nanyi.
3. Lakini watu wakasema, Wewe usitoke nje; kwa maana tukikimbia, hawatatuona sisi kuwa kitu; au tukifa nusu yetu, hawatatuona kuwa kitu; lakini wewe u wa thamani kuliko watu elfu kumi katika sisi; kwa hivyo sasa ni afadhali ukae tayari kutusaidia toka mjini.
4. Mfalme akawaambia, Yaliyo mema machoni penu ndiyo nitakayofanya. Basi mfalme akasimama kando ya lango, na hao watu wakatoka kwa elfu zao na mia zao.
5. Mfalme akawaamuru Yoabu na Abishai na Itai, akasema, Mtendeeni yule kijana, Absalomu, kwa upole kwa ajili yangu. Nao watu wote wakasikia, mfalme alipowaagiza maakida wote katika habari za Absalomu.
6. Hivyo watu wakatoka waende nyikani ili kupigana na Israeli; na vita vikatokea ndani ya msitu wa Efraimu.
7. Watu wa Israeli wakapigwa huko mbele ya watumishi wa Daudi, kukawa na maangamizo makuu huko siku ile, ya watu ishirini elfu.
8. Kwa maana vita vilienea huko juu ya uso wote wa nchi; na siku ile huo msitu ukala watu wengi kuliko wale walioliwa na upanga.
9. Na kwa bahati Absalomu akakutana na watumishi wa Daudi. Naye Absalomu alikuwa amepanda nyumbu wake, na yule nyumbu akapita chini ya matawi manene ya mwaloni mkubwa, hata kichwa chake kikakwama katika mwaloni huo, akanyakuliwa juu kati ya mbingu na nchi; na yule nyumbu aliyekuwa chini yake akaenda mbele.
10. Basi mtu mmoja akaona hayo, akaenda akamwambia Yoabu, akasema, Tazama, mimi nalimwona Absalomu ametundikwa katika mwaloni.
11. Naye Yoabu akamwambia mtu yule aliyempasha habari, Je! Wewe umeona haya; Mbona, basi, hukumpiga hata nchi papo hapo? Nami ningalikupa fedha kumi na mshipi.
12. Yule mtu akamwambia Yoabu, Kama ningalipata fedha elfu mkononi mwangu, hata hivyo singalinyosha mkono wangu juu ya mwana wa mfalme; kwa maana mfalme masikioni mwetu alikuagiza wewe, na Abishai na Itai, akisema, Angalieni sana mtu awaye yote asimguse yule kijana, Absalomu.
13. Na tena, kama ningaliitendea roho yake kwa hila; (wala hapana neno lo lote liwezalo kufichwa mbele ya mfalme); ndipo wewe mwenyewe ungalijitenga.
14. Ndipo Yoabu akasema, Siwezi kungoja na kusema nawe hivi. Akachukua vyemba vitatu mkononi mwake, akamchoma Absalomu moyoni, alipokuwa akali hai katikati ya ule mwaloni.