2 Sam. 11:5-16 Swahili Union Version (SUV)

5. Yule mwanamke akachukua mimba; basi akapeleka na kumwambia Daudi, akasema, Ni mja-mzito.

6. Ndipo Daudi akapeleka kwa Yoabu, akisema, Unipelekee Uria, Mhiti. Naye Yoabu akampeleka Uria kwa Daudi.

7. Uria alipomwendea Daudi, Daudi alimwuliza habari za Yoabu, na habari za watu, na habari za vita.

8. Daudi akamwambia Uria, Haya, shuka nyumbani kwako, ukanawe miguu yako. Basi Uria akatoka katika nyumba ya mfalme, na tunu ya vyakula ikamfuata, iliyotoka kwa mfalme.

9. Lakini Uria akalala mlangoni pa nyumba ya mfalme, pamoja na watumishi wote wa bwana wake, wala hakushuka nyumbani kwake.

10. Watu walipomwambia Daudi ya kwamba, Uria hakushuka nyumbani kwake, Daudi akamwambia Uria, Je! Hukutoka safarini? Mbona hukushuka nyumbani kwako?

11. Naye Uria akamwambia Daudi, Sanduku, na Israeli, na Yuda, wanakaa vibandani; na bwana wangu Yoabu, na watumishi wa bwana wangu, wamepiga kambi waziwazi uwandani; nami niende nyumbani kwangu, kula na kunywa, na kulala na mke wangu? Uishivyo, na kama roho yako iishivyo, mimi sitafanya jambo hili.

12. Basi Daudi akamwambia Uria, Ngoja hapa leo tena, na kesho nitakuacha kwenda zako. Basi Uria akakaa Yerusalemu siku ile, na siku ya pili yake.

13. Naye Daudi akamwalika, akala, akanywa mbele yake; naye akamlevya; hata wakati wa jioni akatoka kwenda kulala kitandani mwake pamoja na watumishi wa bwana wake, lakini hakushuka nyumbani kwake.

14. Hata ikawa asubuhi, Daudi akamwandikia Yoabu waraka, akaupeleka kwa mkono wa Uria.

15. Akaandika katika waraka huo, kusema, Mwekeni Uria mbele ya watu penye vita vikali, kisha ondokeni, mmwache, ili apigwe akafe.

16. Ikawa, Yoabu alipokuwa akiuhusuru mji, akamweka Uria mahali alipojua ya kuwa pana mashujaa.

2 Sam. 11