1. Ikawa baada ya kufa kwake Sauli, hapo Daudi aliporudi katika kuwaua Waamaleki, naye Daudi amekaa siku mbili katika Siklagi;
2. hata siku ya tatu ikawa, tazama! Akaja mtu kutoka kambi ya Sauli, nguo zake zimeraruliwa, tena ana mavumbi kichwani mwake; basi, ikawa alipomfikia Daudi, akaanguka chini, akamsujudia.
3. Daudi akamwambia, Umetoka wapi? Akamwambia, Nimeokoka katika kambi ya Israeli.
4. Daudi akamwambia, Yalikwendaje? Tafadhali uniambie. Akajibu, Watu wamekimbia vitani, tena watu wengi wameanguka wamekufa; hata Sauli naye na Yonathani, mwanawe, wamekufa.
5. Daudi akamwambia yule kijana aliyempa habari, Umejuaje ya kuwa Sauli na Yonathani mwanawe wamekufa?
6. Yule kijana aliyempa habari akasema, Nalikuwapo kwa nasibu juu ya kilima cha Gilboa, na tazama, Sauli alikuwa ameegemea fumo lake; na tazama, magari na wapanda farasi wanamfuatia kwa kasi.