1. Basi hayo yote yalipokwisha, wakatoka Israeli wote waliokuwako waende miji ya Yuda, wakazivunja-vunja nguzo, wakayakata-kata maashera, wakabomoa mahali pa juu na madhabahu katika Yuda yote na Benyamini, katika Efraimu pia na Manase, hata walipokwisha kuviharibu vyote. Ndipo wana wa Israeli wote wakarudi, kila mtu kwa milki yake, mijini kwao.
2. Hezekia akaziweka zamu za makuhani na Walawi kwa zamu zao, kila mtu kwa kadiri ya huduma yake, makuhani na Walawi pia, kwa sadaka za kuteketezwa na kwa sadaka za amani, kutumika, na kushukuru, na kusifu, malangoni mwa matuo ya BWANA.
3. Tena akaweka sehemu ya mfalme ya mali zake kwa sadaka za kuteketezwa, yaani, sadaka za kuteketezwa za asubuhi na jioni, na sadaka za kuteketezwa za sabato, na za mwezi mpya, na sikukuu, kama ilivyoandikwa katika torati ya BWANA.
4. Tena akawaamuru watu waliokaa Yerusalemu, watoe sehemu ya makuhani na Walawi, ili hao wajibidiishe katika torati ya BWANA.
5. Mara ilipotangaa amri, wana wa Israeli wakatoa kwa wingi malimbuko ya nafaka, na divai, na mafuta, na asali, na mazao yote ya mashamba; na zaka za vitu vyote wakazileta nyingi.
6. Nao wana wa Israeli na Yuda, waliokaa mijini mwa Yuda, wakaleta pia zaka za ng’ombe na kondoo, na zaka za vitu vilivyowekwa wakfu, alivyowekewa BWANA, Mungu wao, wakaviweka chungu chungu.
7. Katika mwezi wa tatu wakaanza kuweka misingi ya hizo chungu, wakazimaliza katika mwezi wa saba.
8. Hata walipokuja Hezekia na wakuu, na kuziona zile chungu, wakamhimidi BWANA, na watu wake Israeli.
9. Ndipo Hezekia akaulizana na makuhani na Walawi katika habari ya hizo chungu.
10. Azaria kuhani mkuu, wa nyumba ya Sadoki, akamjibu, akasema, Tangu watu walipoanza kuleta matoleo nyumbani kwa BWANA, tumekula na kushiba, na kusaza tele; kwa kuwa BWANA amewabariki watu wake; na kilichosalia ndiyo akiba hii kubwa.
11. Ndipo Hezekia akaamuru kutengeneza vyumba nyumbani mwa BWANA; wakavitengeneza.