1. Hezekia akatuma wajumbe kwa Israeli wote na Yuda pia; akawaandikia nyaraka Efraimu na Manase, waje nyumbani kwa BWANA Yerusalemu, ili wamfanyie pasaka BWANA, Mungu wa Israeli.
2. Kwa maana mfalme na wakuu wake, na kusanyiko lote katika Yerusalemu walifanya shauri kufanya pasaka mwezi wa pili.
3. Kwa sababu hawakuweza kuifanya wakati ule, kwa kuwa makuhani walikuwa hawajajitakasa wa kutosha, wala watu hawajakusanyika huko Yerusalemu.
4. Likawa neno jema machoni pa mfalme, na kusanyiko lote.
5. Basi wakafanya amri kupiga mbiu kati ya Israeli yote, toka Beer-sheba mpaka Dani, ya kwamba watu waje wamfanyie pasaka BWANA, Mungu wa Israeli, huko Yerusalemu; maana tangu siku nyingi hawakuifanya kama vile ilivyoandikwa.
6. Wakaenda matarishi wenye nyaraka za mfalme na wakuu wake, kati ya Israeli yote na Yuda, na kwa amri ya mfalme, kusema, Enyi wana wa Israeli, mrudieni BWANA, Mungu wa Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, apate kuwarudia waliosalia wenu waliookoka mikononi mwa wafalme wa Ashuru.
7. Wala msiwe kama baba zenu, na kama ndugu zenu, waliomwasi BWANA, Mungu wa baba zao, hata akawatoa kuwa ushangao, kama mwonavyo.
8. Msiwe sasa wenye shingo ngumu kama baba zenu; lakini mjitoe kwa BWANA, mkaingie katika patakatifu pake, alipopatakasa milele, mkamtumikie BWANA, Mungu wenu, hasira yake kali iwageukie mbali.
9. Kwa kuwa mkimrudia BWANA, ndugu zenu na watoto wenu watahurumiwa machoni pa hao waliowachukua mateka, nao watairudia nchi hii; kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, ndiye mwenye neema, na mwenye rehema, wala hatawageuzia mbali uso wake, mkimrudia.
10. Basi matarishi wakapita mji kwa mji kati ya nchi ya Efraimu na Manase, hata kufika Zabuloni; lakini waliwacheka-cheka, na kuwadhihaki.