2 Nya. 29:25-34 Swahili Union Version (SUV)

25. Akawasimamisha Walawi nyumbani mwa BWANA wenye matoazi, wenye vinanda, na wenye vinubi, kama alivyoamuru Daudi, na Gadi mwonaji wa mfalme, na Nathani nabii; kwani BWANA aliamuru hivi kwa manabii wake.

26. Wakasimama Walawi wenye vinanda vya Daudi, na makuhani wenye mapanda.

27. Hezekia akaamuru kutoa sadaka ya kuteketezwa madhabahuni. Na wakati ilipoanza sadaka hiyo ya kuteketezwa, ukaanza na huo wimbo wa BWANA, na mapanda, pamoja na vinanda vya Daudi mfalme wa Israeli.

28. Na kusanyiko lote wakaabudu, waimbaji wakaimba, wenye mapanda wakapiga; haya yote yakaendelea hata ilipomalizika sadaka ya kuteketezwa.

29. Hata walipokwisha kutoa sadaka, mfalme, na hao wote waliokuwapo naye, wakasujudia, wakaabudu.

30. Tena Hezekia mfalme na wakuu wakawaamuru Walawi, wamwimbie BWANA sifa kwa maneno ya Daudi, na ya Asafu mwonaji. Wakaimba sifa kwa furaha, wakainama vichwa, wakaabudu.

31. Ndipo Hezekia akajibu, akasema, Sasa mmejifanya wakfu kwa BWANA, karibuni mkalete dhabihu na matoleo ya shukrani nyumbani mwa BWANA. Basi kusanyiko wakaleta dhabihu na matoleo ya shukrani; na wote wenye moyo wa ukarimu, wakaleta sadaka za kuteketezwa.

32. Na hesabu ya sadaka hizo za kuteketezwa walizozileta kusanyiko ikawa ng’ombe waume sabini, kondoo waume mia, na wana-kondoo mia mbili; hao wote walikuwa ni sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA.

33. Na vitu vitakatifu vilikuwa ng’ombe mia sita, na kondoo elfu tatu.

34. Lakini makuhani walikuwa wachache, wasiweze kuchuna sadaka zote za kuteketezwa; basi ndugu zao Walawi wakawasaidia, hata ilipokwisha kazi, na hata makuhani walipojitakasa; kwa kuwa Walawi walikuwa wenye mioyo ya adili kwa kujitakasa kuliko makuhani.

2 Nya. 29