2 Nya. 25:5-16 Swahili Union Version (SUV)

5. Tena Amazia akawakusanya Yuda, akawaweka sawasawa na nyumba za baba zao chini ya maakida wa maelfu, na maakida wa mamia, naam, Yuda pia, na Benyamini; tangu wenye miaka ishirini na zaidi akawahesabu, akawaona kuwa watu wateule mia tatu elfu, wawezao kwenda vitani, waliozoea mkuki na ngao.

6. Akaajiri pia watu mashujaa mia elfu wa Israeli kwa talanta mia za fedha.

7. Lakini mtu wa Mungu akamjia, akasema, Ee mfalme, usiwaache jeshi la Israeli waende nawe; kwa kuwa BWANA hayupo pamoja na Israeli, yaani, wana wote wa Efraimu.

8. Lakini ukitaka kwenda, haya, jitie nguvu upigane; Mungu atakuangusha mbele ya adui; maana Mungu anazo nguvu za kusaidia, na kuangusha.

9. Amazia akamwambia mtu wa Mungu, Lakini tuzifanyieje zile talanta mia nilizowapa jeshi la Israeli? Mtu wa Mungu akajibu, BWANA aweza kukupa zaidi sana kuliko hizo.

10. Ndipo Amazia akawafarakisha jeshi lililomjia kutoka Efraimu, ili warudi kwao; kwa hiyo ikawaka sana hasira yao juu ya Yuda, nao wakarudi kwao wenye hasira kali.

11. Amazia akapiga moyo konde, akawaongoza watu wake, akaenda mpaka Bonde la Chumvi, akawapiga katika wana wa Seiri watu elfu kumi.

12. Na elfu kumi wengine, ambao wana wa Yuda waliwachukua wali hai, wakawaleta juu ya jabali, wakawaangusha toka juu ya jabali, hata wakavunjika-vunjika wote.

13. Lakini wale watu wa jeshi, aliowarudisha Amazia, wasiende naye vitani, hao wakaiteka miji ya Yuda, tangu Samaria mpaka Beth-horoni, wakawapiga watu elfu tatu, wakachukua nyara nyingi.

14. Basi ikawa, Amazia alipokwisha rudi kutoka kuwaua Waedomi, alileta miungu ya wana wa Seiri, akaisimamisha kuwa miungu yake, akajiinama mbele yao, akaifukizia uvumba.

15. Kwa hiyo hasira ya BWANA ikawaka juu ya Amazia, akampelekea nabii, aliyemwambia, Mbona umeitafuta miungu ya watu, isiyowaokoa watu wao mkononi mwako?

16. Ikawa, aliposema naye, mfalme akamwambia, Je! Tumekutia wewe kuwa mshauri wa mfalme? Nyamaza; kwa nini upigwe? Ndipo yule nabii akaacha, akasema, Najua ya kuwa Mungu amekusudia kukuangamiza, kwa sababu umeyafanya haya, wala hukulisikiliza shauri langu.

2 Nya. 25