2 Fal. 8:1-16 Swahili Union Version (SUV)

1. Basi Elisha alikuwa amemwambia yule mwanamke, ambaye alimfufulia mwanawe, akasema, Ondoka, ukaende wewe na jamaa yako, ukae hali ya kigeni utakakoweza kukaa; kwa sababu BWANA ameiita njaa; nayo itakuja juu ya nchi hii muda wa miaka saba.

2. Akaondoka yule mwanamke, akafanya kama alivyosema mtu wa Mungu; akaenda, yeye na jamaa yake, akakaa katika nchi ya Wafilisti miaka saba.

3. Ikawa miaka saba ilipoisha, yule mwanamke akarudi kutoka nchi ya Wafilisti; akatokea amlilie mfalme kwa ajili ya nyumba yake na shamba lake.

4. Basi mfalme alikuwa akizungumza na Gehazi, mtumishi wa mtu wa Mungu, akinena, Uniambie, nakusihi, mambo makuu yote aliyoyafanya Elisha.

5. Ikawa, alipokuwa katika kumwambia mfalme jinsi alivyomfufua mtu aliyekufa, tazama, huyo mwanamke aliyemfufulia mwanawe, alimlilia mfalme kwa ajili ya nyumba yake na shamba lake. Gehazi akasema, Bwana wangu mfalme, huyu ndiye mwanamke, na huyu ndiye mwanawe, ambaye Elisha alimfufua.

6. Na mfalme alipomwuliza yule mwanamke, yeye akamweleza. Basi mfalme akamtolea akida, akasema, Mrudishie yote aliyokuwa nayo, na mapato yote ya shamba lake tangu siku aliposafiri, hata leo.

7. Kisha, Elisha akaenda Dameski; na Ben-hadadi, mfalme wa Shamu, alikuwa hawezi; akaambiwa ya kwamba, Yule mtu wa Mungu amefika hapa.

8. Mfalme akamwambia Hazaeli, Chukua zawadi mkononi mwako, ukaende ili kumlaki yule mtu wa Mungu, ukamwulize BWANA kwa kinywa chake, kusema, Je! Nitapona ugonjwa huu?

9. Basi Hazaeli akaenda kumlaki, akachukua zawadi mkononi mwake, za kila kitu chema kilichopatikana Dameski, kiasi cha mizigo ya ngamia arobaini, akaenda, akasimama mbele yake akasema, Mwana wako Ben-hadadi, mfalme wa Shamu, amenituma kwako, kusema, Je nitapona ugonjwa huu?

10. Elisha akamwambia, Enenda, ukamwambie, Bila shaka utapona; lakini BWANA amenionyesha ya kwamba bila shaka atakufa.

11. Akamkazia macho hata akatahayari; na yule mtu wa Mungu akalia machozi.

12. Hazaeli akasema, Bwana wangu analilia nini? Akajibu, Kwa sababu nayajua mabaya utakayowatenda wana wa Israeli; utazichoma moto ngome zao, utawaua vijana wao kwa upanga, utawaseta-seta watoto wao wachanga na wanawake wao wenye mimba utawapasua.

13. Hazaeli akasema, Lakini mimi mtumwa wako ni nani, mimi niliye mbwa tu, hata nifanye jambo hili kubwa? Elisha akajibu, BWANA amenionyesha ya kwamba wewe utakuwa mfalme juu ya Shamu.

14. Ndipo akamwacha Elisha, akarudi kwa bwana wake; naye akamwambia, Elisha alikuambiaje? Akajibu, Aliniambia ya kuwa bila shaka utapona.

15. Ikawa siku ya pili yake, akatwaa tandiko la kitanda, akalichovya katika maji, akalitandaza juu ya uso wake, hata akafa. Na Hazaeli akatawala badala yake.

16. Katika mwaka wa tano wa Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli, [Yehoshafati alipokuwa mfalme wa Yuda], alianza kutawala Yehoramu mwana wa Yehoshafati mfalme wa Yuda.

2 Fal. 8