5. Lakini mmojawapo alipokuwa katika kukata boriti, chuma cha shoka kikaanguka majini; akalia, akasema, Ole wangu! Bwana wangu, kwani kiliazimiwa kile.
6. Mtu wa Mungu akasema, Kilianguka wapi? Akamwonyesha mahali. Akakata kijiti, akakitupa pale pale, chuma kikaelea.
7. Akasema, Kiokote. Basi akanyosha mkono, akakitwaa.
8. Basi, mfalme wa Shamu alikuwa akifanya vita na Israeli. Akafanya mashauri na watumishi wake, akasema, Kituo changu kitakuwapo mahali fulani.
9. Yule mtu wa Mungu akapeleka habari kwa mfalme wa Israeli, kusema, Jihadhari, usipite mahali fulani; kwa sababu ndiko wanakoshukia Washami.
10. Mfalme wa Israeli akapeleka watu mpaka mahali pale alipoambiwa na yule mtu wa Mungu, na kuhadharishwa; akajiokoa nafsi yake, si mara moja, wala si mara mbili.
11. Basi mfalme wa Shamu moyo wake ukamfadhaika sana kwa ajili ya jambo hili; akawaita watumishi wake, akawaambia, Je! Hamtanionyesha, ni mtu yupi miongoni mwenu aliye upande wa mfalme wa Israeli?
12. Mmojawapo wa watumishi wake akasema, La, bwana wangu, mfalme; lakini Elisha, yule nabii aliye katika Israeli, humwambia mfalme wa Israeli maneno uyanenayo katika chumba chako cha kulala.
13. Akasema, Enendeni, mkamwangalie aliko, nipate kupeleka watu kwenda kumchukua. Akaambiwa ya kwamba, Tazama, yuko Dothani.
14. Kwa hiyo akapeleka huko farasi, na magari, na jeshi kubwa; wakafika usiku, wakauzingira mji ule pande zote.