16. Naye Yosia alipogeuka, aliyaona makaburi yale yaliyokuwako huko, juu ya mlima; akatuma watu, akaitoa ile mifupa katika yale makaburi, akaiteketeza juu ya madhabahu, akainajisi, sawasawa na lile neno la BWANA, alilolinena yule mtu wa Mungu, aliyetamka mambo hayo.
17. Kisha akasema, Ni kumbukumbu la nani, hili ninaloliona? Na watu wa mji wakamwambia, Ni kaburi la yule mtu wa Mungu, aliyetoka Yuda, akayanena mambo hayo uliyoyatenda wewe juu ya madhabahu ya Betheli.
18. Akasema, Mwacheni; mtu awaye yote asiiondoe mifupa yake. Basi wakaiacha mifupa yake, pamoja na mifupa ya yule nabii aliyetoka Samaria.
19. Na nyumba zote pia za mahali pa juu palipokuwa katika miji ya Samaria, wafalme wa Israeli walizozifanya, ili kumkasirisha BWANA, Yosia aliziondoa, akazitenda kwa mfano wa mambo yote aliyoyatenda katika Betheli.
20. Akawaua na makuhani wote wa mahali pa juu waliokuwako huko, juu ya madhabahu, akateketeza mifupa ya watu juu yake; kisha akarejea Yerusalemu.
21. Naye mfalme akawaamuru watu wote, akasema, Mfanyieni BWANA, Mungu wenu, pasaka, kama ilivyoandikwa katika kitabu hiki cha agano.
22. Hakika yake haikufanyika pasaka kama hiyo, tangu zamani za waamuzi waliowaamua Israeli, wala katika zamani za wafalme wa Israeli, wala za wafalme wa Yuda.
23. Bali katika mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yosia ilifanyika pasaka hii kwa BWANA ndani ya Yerusalemu.
24. Tena wenye pepo wa utambuzi, na wachawi, na vinyago, na sanamu, na machukizo yote yaliyoonekana katika nchi ya Yuda na katika Yerusalemu, Yosia akayaondoa yote, ili apate kuyathibitisha maneno ya torati yaliyoandikwa katika kile kitabu alichokiona Hilkia kuhani ndani ya nyumba ya BWANA.
25. Kabla ya huyo hapakuwa na mfalme mfano wake, aliyemwelekea BWANA kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kwa nguvu zake zote, sawasawa na sheria zote za Musa; wala baada yake hakuinuka mmoja mfano wake yeye.
26. Walakini BWANA hakuuacha ukali wa ghadhabu yake nyingi, ambayo kwayo hasira yake iliwaka juu ya Yuda, kwa sababu ya machukizo yote ambayo Manase amemchukiza.
27. BWANA akasema Nitawahamisha Yuda pia mbali nami, kama nilivyowahamisha Israeli, nami nitautupa mji huu niliouchagua, naam, Yerusalemu, na nyumba ile niliyoinena, Jina langu litakuwa humo.
28. Basi mambo yote ya Yosia yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
29. Katika siku zake, Farao-neko, mfalme wa Misri, akakwea ili kupigana na mfalme wa Ashuru, akafika mto Frati; naye mfalme Yosia akaenda kupigana naye; naye mfalme wa Misri akamwua huko Megido, hapo alipoonana naye.
30. Watumishi wake wakamchukua garini, amekwisha kufa, kutoka Megido, wakamleta Yerusalemu, wakamzika katika kaburi lake mwenyewe. Watu wa nchi wakamtwaa Yehoahazi mwana wa Yosia, wakamtia mafuta, wakamtawaza awe mfalme badala ya baba yake.
31. Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala; akatawala miezi mitatu katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Hamutali binti Yeremia wa Libna.