7. Tazama, nitatia roho ya hofu ndani yake, naye atasikia kivumi, na kuirudia nchi yake mwenyewe; nami nitamwangusha kwa upanga katika nchi yake mwenyewe.
8. Basi yule amiri akarudi, akamkuta mfalme wa Ashuru, anapigana na Libna; maana alikuwa amesikia ya kwamba ameondoka, akaacha Lakishi.
9. Na aliposikia habari ya Tirhaka mfalme wa Kushi, ya kwamba, Tazama, ametoka ili kupigana nawe; alituma wajumbe kwa Hezekia mara ya pili, kusema,
10. Mwambieni Hezekia, mfalme wa Yuda, maneno haya, mkisema, Asikudanganye Mungu wako unayemtumaini, akisema, Yerusalemu hautatiwa katika mikono ya mfalme wa Ashuru.
11. Tazama, umesikia ni mambo gani wafalme wa Ashuru waliyozitenda nchi zote, kwa kuziangamiza kabisa; je! Utaokoka wewe?
12. Je! Miungu ya mataifa wale, ambao baba zangu waliwaangamiza, imewaokoa? Yaani, Gozani, na Harani, na Resefu, na wana wa Adini waliokuwa katika Telasari?
13. Yuko wapi mfalme wa Hamathi, na mfalme wa Arpadi, na mfalme wa mji wa Sefarvaimu, na wa Hena, na wa Iva?
14. Basi Hezekia akaupokea waraka katika mikono ya wale wajumbe, akausoma; kisha Hezekia akapanda, akaingia katika nyumba ya BWANA, akaukunjua mbele za BWANA.
15. Naye Hezekia akaomba mbele za BWANA, akasema, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, ukaaye juu ya makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia; wewe ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi.
16. Tega sikio lako, Ee BWANA, usikie; fumbua macho yako, Ee BWANA, uone; uyasikie maneno ya Senakeribu, ambayo amemtuma mtu aje nayo ili kumtukana Mungu aliye hai.
17. Ni kweli, BWANA, wafalme wa Ashuru wamewaharibu mataifa na nchi zao,
18. na kuitupa miungu yao motoni; kwa maana haikuwa miungu, bali ni kazi ya mikono ya wanadamu; ilikuwa miti na mawe tu, ndiyo sababu wakaiharibu.
19. Basi sasa, Ee BWANA, Mungu wetu, utuokoe na mkono wake, nakusihi, ili kwamba falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe BWANA Mungu, wewe peke yako.
20. Ndipo Isaya, mwana wa Amozi, akapeleka ujumbe kwa Hezekia, akisema, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa kuwa umeniomba juu ya Senakeribu, mfalme wa Ashuru, mimi nimekusikia.
21. Tamko alilolitamka BWANA katika habari zake ndilo hili, Bikira, binti Sayuni, amekudharau, na kukudhihaki sana; binti Yerusalemu ametikisa kichwa chake juu yako.
22. Ni nani uliyemshutumu na kumtukana? Umeinua sauti yako juu ya nani, na kuinua macho yako juu? Juu ya Mtakatifu wa Israeli.
23. Kwa vinywa vya wajumbe wako umemshutumu Bwana, ukasema, Kwa wingi wa magari yangu nimepanda juu ya vilele vya milima, mpaka mahali pa ndani pa Lebanoni. Nami nitaikata mierezi yake mirefu, na misunobari yake mizuri; nami nitaingia ndani ya makazi yake yaliyo mbali sana, na msitu wa shamba lake lizaalo sana.
24. Nimechimba na kunywa maji mageni, na kwa nyayo za miguu yangu nitaikausha mito yote ya Misri.
25. Je! Hukusikia wewe ya kuwa mimi ndimi niliyeyatenda hayo tokea zamani, na kuyafanya tokea siku za kale? Sasa mimi nimelitimiza jambo hili, iwe kazi yako kuangamiza miji yenye boma, hata ikawe chungu na magofu.
26. Ndiyo sababu wenyeji wao walikuwa na nguvu chache, wakafadhaika, na kuhangaika; wakawa kama majani ya mashamba, kama miche mibichi, kama majani juu ya dari, na kama ngano iliyokaushwa kabla haijaiva.