21. Sasa tazama, unaitumainia fimbo ya mwanzi huu uliopondeka, yaani, Misri, ambayo mtu akiitegemea, humwingia mkononi na kumchoma; ndivyo alivyo Farao, mfalme wa Misri, kwa wote wamtumainio.
22. Lakini mkiniambia, Tunamtumaini BWANA, Mungu wetu; je! Si yeye ambaye Hezekia ameondoa mahali pake pa juu, na madhabahu zake, akawaambia watu wa Yuda na Yerusalemu, Sujuduni mbele ya madhabahu hii hapa Yerusalemu?
23. Basi sasa, tafadhali mpe bwana wangu, mfalme wa Ashuru, dhamana, nami nitakupa farasi elfu mbili, ikiwa wewe kwa upande wako waweza kupandisha watu juu yao.
24. Wawezaje, basi, kurudisha nyuma uso wa akida mmoja wa watumishi walio wadogo wa bwana wangu, na kuitumainia Misri upewe magari na farasi?
25. Je! Nimepanda mimi, ili kupigana na mahali hapa na kupaangamiza, bila shauri la BWANA? BWANA ndiye aliyeniambia, Panda upigane na nchi hii na kuiangamiza.
26. Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, na Shebna, na Yoa, wakamwambia yule amiri, Tafadhali, sema na watumishi wako kwa lugha ya Kiashuri; maana tunaifahamu; wala usiseme nasi kwa lugha ya Kiyahudi, masikioni mwa hao watu walio ukutani.
27. Lakini yule amiri akawaambia, Je! Bwana wangu amenituma kwa bwana wako, na kwako wewe, niseme maneno haya? Je! Hakunituma kwa watu hawa walio ukutani, ili wale mavi yao wenyewe na kunywa mkojo wao pamoja nanyi?
28. Kisha yule amiri akasimama akalia kwa sauti kuu kwa lugha ya Kiyahudi, akasema, Lisikieni neno la mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru.
29. Mfalme asema hivi, Hezekia asiwadanganye; kwa maana, hataweza kuwaokoa katika mkono wake.
30. Wala Hezekia asiwatumainishe katika BWANA, akisema, Hakika BWANA atatuokoa, wala mji huu hautatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru.
31. Msimsikilize Hezekia; kwa sababu mfalme wa Ashuru asema hivi, Fanyeni suluhu na mimi, mkatoke mnijie; mkale kila mtu matunda ya mzabibu wake na matunda ya mtini wake, mkanywe kila mmoja maji ya birika lake mwenyewe;
32. hata nije nikawachukue mpaka nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai, nchi ya chakula na mashamba ya mizabibu, nchi ya mafuta ya mzeituni na asali, ili mpate kuishi, msife; wala msimsikilize Hezekia, awadanganyapo, akisema, BWANA atatuokoa.
33. Je! Yuko mungu mmoja wa mataifa aliyewaokoa watu wake wakati wo wote na mkono wa mfalme wa Ashuru?
34. Iko wapi miungu ya Hamathi, na ya Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu, na ya Hena, na ya Iva? Je! Imeuokoa Samaria na mkono wangu?
35. Katika miungu ya nchi hizi zote, ni miungu gani iliyookoa nchi yao na mkono wangu, hata BWANA auokoe Yerusalemu na mkono wangu?