2 Fal. 11:1-14 Swahili Union Version (SUV)

1. Na Athalia, mama yake Ahazia, alipoona ya kuwa mwanawe amekufa, akainuka, akawaharibu wazao wote wa kifalme.

2. Ila Yehosheba, binti wa mfalme Yehoramu, umbu lake Ahazia, akamtwaa Yoashi mwana wa Ahazia, akamwiba miongoni mwa hao wana wa mfalme waliouawa, yeye na mlezi wake, na kuwatia katika chumba cha kulala; wakamficha usoni pa Athalia, basi kwa hiyo hakuuawa.

3. Alikuwako pamoja naye, amefichwa nyumbani mwa BWANA, miaka sita. Naye Athalia akaitawala nchi.

4. Hata mwaka wa saba Yehoyada akatuma, na kuwaleta wakuu wa mamia, wa Wakari, na wa walinzi, akawaleta kwake ndani ya nyumba ya BWANA; akapatana nao, akawaapisha nyumbani mwa BWANA, akawaonyesha huyo mwana wa mfalme.

5. Akawaamuru, akasema, Hili ndilo neno mtakalolifanya; theluthi yenu, mtakaoingia siku ya sabato, mtayalinda malinzi ya nyumba ya mfalme;

6. na theluthi mtakuwapo mlangoni pa Suri; na theluthi langoni nyuma ya walinzi; hivyo mtayalinda malinzi ya nyumba, kuzuia watu wasiingie.

7. Na sehemu mbili zenu, yaani, wote watokao siku ya sabato, mtayalinda malinzi ya nyumba ya BWANA kumzunguka mfalme.

8. Mtamzunguka mfalme pande zote, kila mtu mwenye silaha zake mkononi; naye awaye yote aingiaye ndani ya safu auawe; mkafuatane na mfalme, akitoka na akiingia.

9. Nao wakuu wa mamia wakafanya sawasawa na yote aliyowaamuru Yehoyada kuhani; wakawatwaa kila mtu watu wake, hao watakaoingia sabato, nao watakaotoka sabato, wakaja kwa Yehoyada kuhani.

10. Naye yule kuhani akawapa wakuu wa mamia mikuki na ngao zilizokuwa za mfalme Daudi, zilizokuwamo nyumbani mwa BWANA.

11. Walinzi wakasimama, kila mtu na silaha zake mkononi, kutoka pembe ya kuume ya nyumba mpaka pembe ya kushoto ya nyumba, kando ya madhabahu na nyumba, wakimzunguka mfalme pande zote.

12. Ndipo akamleta nje mwana wa mfalme, akamvika taji, na kumpa ushuhuda; wakamfanya mfalme, wakamtia mafuta; wakapiga makofi, wakasema, mfalme na aishi.

13. Na Athalia alipoisikia sauti ya walinzi na ya watu, aliingia kwa watu nyumbani kwa BWANA;

14. akatazama, na tazama, mfalme amesimama karibu na nguzo kama ilivyokuwa desturi, nao wakuu na wapiga baragumu karibu na mfalme; na watu wote wa nchi wakafurahi, wakapiga baragumu. Ndipo Athalia akararua mavazi yake, akalia, Fitina! Fitina!

2 Fal. 11