1 Sam. 6:1-12 Swahili Union Version (SUV)

1. Basi, hilo sanduku la BWANA lilikuwamo katika nchi ya Wafilisti muda wa miezi saba.

2. Nao Wafilisti wakawaita makuhani na waaguzi, wakasema, Tulifanyieje sanduku la BWANA? Tuonyesheni jinsi tuwezavyo kulirudisha mahali pake.

3. Nao wakajibu, Mkilirudisha hilo sanduku la Mungu wa Israeli, msilirudishe kitupu; lakini msikose kumpelekea na matoleo ya kosa; hivyo mtapona, tena mtafunuliwa ni kwa sababu gani mkono wake haukuondolewa kwenu.

4. Ndipo wakauliza, Na hayo matoleo ya kosa yatakuwa ya namna gani, hayo tutakayompelekea? Nao wakajibu, Na yawe majipu ya dhahabu matano, na panya wa dhahabu watano, sawasawa na idadi ya mashehe wa Wafilisti; kwa kuwa tauni moja ilikuwa juu yenu nyote, na juu ya mashehe wenu.

5. Kwa hiyo mtafanyiza sanamu za majipu yenu, na sanamu za panya wenu waiharibuo nchi; nanyi mtamtukuza huyo Mungu wa Israeli; huenda ataupunguza uzito wa mkono wake juu yenu, na juu ya miungu yenu, na juu ya nchi yenu.

6. Mbona, basi, mnaifanya migumu mioyo yenu, kama vile wale Wamisri, naye yule Farao, walivyoifanya migumu mioyo yao? Hata na hao, hapo alipokwisha kuwadhihaki, je! Hawakuwaruhusu watu, nao wakaenda zao?

7. Basi sasa jifanyizieni gari jipya, mtwae na ng’ombe wake wawili wakamwao, ambao hawajafungwa nira, nanyi mkawafunge hao ng’ombe garini, na kuwaondoa ndama zao na kuwatia zizini;

8. kisha, litwaeni hilo sanduku la BWANA, na kuliweka juu ya gari; na hivyo vitu vya dhahabu, mtakavyompelekea kuwa matoleo ya kosa, mvitie katika kasha kando yake; mkalipeleke sanduku, lipate kwenda.

9. Kisha angalieni, likikwea kwa njia ya mpakani mwake kwenda Beth-shemeshi, basi, ndiye aliyetutenda uovu huo mkuu; la, sivyo, ndipo tutakapojua ya kwamba si mkono wake uliotupiga; ilikuwa ni ajali iliyotupata.

10. Basi watu wale walifanya hivyo; wakatwaa ng’ombe wawili wakamwao, wakawafunga garini, na ndama zao wakawafunga zizini;

11. kisha wakaliweka sanduku la BWANA juu ya gari, pamoja na kasha lenye panya wa dhahabu na sanamu za majipu yao.

12. Na hao ng’ombe wakashika njia moja kwa moja kwenda Beth-shemeshi; wakaiandama njia ya barabara, wakaenda wakilia, lakini hawakugeukia upande wa kuume wala wa kushoto; na mashehe wa Wafilisti wakawafuata hata kuufikia mpaka wa Beth-shemeshi.

1 Sam. 6