8. Ndipo Abishai akamwambia Daudi, Mungu amemtia adui yako mikononi mwako leo; basi, niache nimpige kwa hilo fumo hata nchi kwa pigo moja, sitampiga mara ya pili.
9. Lakini Daudi akamwambia Abishai, Usimwangamize; kwani ni nani awezaye kuunyosha mkono wake juu ya masihi wa BWANA, naye akawa hana hatia?
10. Daudi akasema, Aishivyo BWANA, BWANA atampiga; au siku yake ya kufa itampata; atashuka kwenda vitani na kupotea.
11. Hasha! Nisiunyoshe mkono wangu juu ya masihi wa BWANA; lakini sasa tafadhali twaa hili fumo lililo kichwani pake, na hili gudulia la maji, nasi twende zetu.
12. Basi Daudi akalitwaa lile fumo, na lile gudulia la maji, kichwani pa Sauli; nao wakaenda zao, wala hapana mtu aliyeliona jambo hili wala kulijua, wala kuamka; maana wote walikuwa wamelala; kwa kuwa usingizi mzito kutoka kwa BWANA umewaangukia.
13. Kisha Daudi akaenda ng’ambo ya pili, akasimama juu ya kilima, mbali sana; palipokuwapo nafasi tele katikati yao;
14. naye Daudi akawapigia kelele watu wale, na Abneri, mwana wa Neri, akasema, Abneri, hujibu? Ndipo Abneri akajibu, akasema, U nani wewe unayemlilia mfalme?
15. Naye Daudi akamwambia Abneri, Wewe si mtu shujaa? Tena ni nani aliye sawa na wewe katika Israeli? Mbona, basi, hukumlinda bwana wako, huyo mfalme? Kwa maana mtu mmoja aliingia ili amwangamize mfalme, bwana wako?
16. Jambo hili ulilolitenda si jema. Aishivyo BWANA, mmestahili kufa, kwa sababu hamkumlinda bwana wenu, masihi wa BWANA. Haya basi! Tazameni, liko wapi fumo la mfalme, na gudulia la maji lililokuwa kichwani pake?