33. Sauli akamtupia mkuki wake ili kumpiga; basi Yonathani akajua ya kuwa baba yake ameazimu kumwua Daudi.
34. Basi Yonathani akaondoka pale mezani, mwenye hasira kali, wala hakula chakula siku ya pili ya mwezi, kwa sababu alimhuzunikia Daudi sana, na kwa sababu baba yake amemwaibisha.
35. Hata asubuhi Yonathani akatoka kwenda shambani wakati ule alioagana na Daudi, na mtoto mdogo alikuwa pamoja naye.
36. Akamwambia mtoto wake, Piga mbio, ukaitafute mishale niipigayo. Na yule mtoto alipokuwa akipiga mbio, akapiga mshale, ukapita juu yake.
37. Na mtoto alipofika penye ule mshale alioupiga Yonathani, Yonathani akampigia mtoto kelele, akasema, Je! Mshale si huko mbele yako?
38. Yonathani akampigia mtoto kelele, Haya! Hima! Usikawie. Mtoto wa Yonathani akaikusanya mishale, akaenda kwa bwana wake.
39. Lakini yule mtoto hakujua lo lote. Yonathani na Daudi ndio walioijua habari yenyewe.
40. Naye Yonathani akampa mtoto silaha zake, akamwambia, Nenda, ukazichukue mjini.
41. Basi mara alipokuwa amekwisha ondoka yule mtoto, mara Daudi akatoka mahali pale karibu na kile kichuguu, akaanguka kifudifudi, akajiinama mara tatu; nao wakabusiana, wakaliliana, hata Daudi akazidi.
42. Naye Yonathani akamwambia Daudi, Enenda kwa amani; kwa maana sisi sote wawili tumeapiana kwa jina la BWANA ya kwamba, BWANA atakuwa kati ya mimi na wewe, na kati ya uzao wangu na uzao wako milele. Daudi akaondoka, akaenda zake; Yonathani naye akaenda zake mjini.