1 Sam. 20:1-7 Swahili Union Version (SUV)

1. Kisha Daudi akatoka Nayothi huko Rama, akakimbia, akaenda kwa Yonathani, akasema mbele yake, Nimefanya nini? Uovu wangu ni nini? Dhambi yangu mbele ya baba yako ni nini, hata akaitaka roho yangu?

2. Naye akamwambia, Hasha! Hutakufa; angalia, baba yangu hatendi neno kubwa wala dogo bila kuifunulia mimi, na baba yangu ana sababu gani ya kunificha jambo hili? Sivyo usemavyo.

3. Daudi akaapa, akasema, Baba yako anajua sana ya kuwa nimeona kibali machoni pako, naye asema, Yonathani asilijue neno hili, asije akahuzunika; lakini ni kweli, aishivyo BWANA, na iishivyo roho yako, iko hatua moja tu kati ya mimi na mauti.

4. Ndipo Yonathani akamwambia Daudi, Kadiri roho yako itakavyo, nitakutendea.

5. Naye Daudi akamwambia Yonathani, Tazama, kesho ni mwandamo wa mwezi, nami hainipasi kukosa kuketi chakulani pamoja na mfalme; lakini niache nijifiche bondeni hata siku ya tatu jioni.

6. Baba yako akiona ya kuwa sipo basi sema, Daudi alitaka sana nimpe ruhusa, aende upesi Bethlehemu, mji wake, kwa maana iko huko dhabihu ya mwaka kwa ajili ya jamaa yake yote.

7. Basi, akisema, Ni vema, mimi mtumishi wako nitakuwa na amani; bali akikasirika, ujue ya kuwa amekusudia kutenda jambo baya.

1 Sam. 20