1 Sam. 2:19-29 Swahili Union Version (SUV)

19. Tena mamaye humfanyizia kanzu ndogo, na kumletea mwaka kwa mwaka, hapo alipokwea pamoja na mumewe ili kutoa dhabihu kila mwaka.

20. Naye Eli akambariki Elkana na mkewe, akasema, BWANA na akupe uzao kwa mwanamke huyu, badala ya azimo aliloazimiwa BWANA. Kisha wakaenda nyumbani kwao.

21. Naye BWANA akamwangalia Hana, naye akachukua mimba, akazaa watoto, wa kiume watatu na wa kike wawili. Naye huyo mtoto Samweli akakua mbele za BWANA.

22. Basi Eli alikuwa mzee sana; naye alisikia habari za mambo yote ambayo wanawe waliwatenda Waisraeli; na jinsi walivyolala na wanawake waliokuwa wakitumika mlangoni pa hema ya kukutania.

23. Akawaambia, Mbona mnatenda mambo kama hayo? Maana nasikia habari za matendo yenu mabaya kwa watu hawa wote.

24. Sivyo hivyo, wanangu, kwa maana habari hii ninayoisikia si habari njema; mnawakosesha watu wa BWANA.

25. Mtu mmoja akimkosa mwenzake, Mungu atamhukumu; lakini mtu akimkosa BWANA, ni nani atakayemtetea? Lakini hawakuisikia sauti ya baba yao, kwa sababu BWANA amekusudia kuwaua.

26. Na yule mtoto, Samweli, akazidi kukua akapata kibali kwa BWANA, na kwa watu pia.

27. Kisha mtu wa Mungu akamwendea Eli, akamwambia, BWANA asema hivi, Je! Mimi sikujidhihirisha nafsi yangu kwa nyumba ya baba yako, walipokuwa katika Misri, wakiitumikia nyumba ya Farao?

28. Je! Sikumchagua yeye katika kabila zote za Israeli, ili awe kuhani wangu, apande madhabahuni kwangu; na kufukiza uvumba, na kuvaa naivera mbele zangu? Nami sikuwapa watu wa mbari ya baba yako dhabihu zote za wana wa Israeli zilizotolewa kwa moto?

29. Kwa nini basi mnaipiga teke dhabihu yangu na sadaka yangu nilizoziamuru katika maskani yangu; ukawaheshimu wanao kuliko mimi, mpate kujinenepesha kwa sadaka zote za watu wangu Israeli zilizo njema?

1 Sam. 2