1 Sam. 18:3-20 Swahili Union Version (SUV)

3. Nao Yonathani na Daudi wakaahidiana, kwa kuwa alimpenda kama roho yake mwenyewe.

4. Ndipo Yonathani akalivua joho alilokuwa amelivaa, akampa Daudi, na mavazi yake, hata na upanga wake pia, na upinde wake, na mshipi wake.

5. Basi Daudi akatoka kwenda kila mahali alikotumwa na Sauli, akatenda kwa akili; Sauli akamweka juu ya watu wa vita; jambo hili likawa jema machoni pa watu wote, na machoni pa watumishi wa Sauli pia.

6. Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda.

7. Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema,Sauli amewaua elfu zake,Na Daudi makumi elfu yake.

8. Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme?

9. Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile.

10. Ikawa siku ya pili yake, roho mbaya kutoka kwa Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, naye akatabiri ndani ya nyumba. Basi Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake kama siku zote; naye Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake.

11. Mara Sauli akautupa ule mkuki; maana alisema, Nitampiga Daudi hata ukutani. Daudi akaepa, akatoka mbele yake, mara mbili.

12. Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu BWANA alikuwa pamoja naye, ila amemwacha Sauli.

13. Kwa ajili ya hayo Sauli akamwondosha kwake, akamfanya awe akida wake juu ya askari elfu; naye akatoka na kuingia mbele ya watu.

14. Naye Daudi akatenda kwa busara katika njia zake zote naye BWANA alikuwa pamoja naye.

15. Sauli alipoona ya kwamba alitenda kwa busara sana, yeye alimwogopa.

16. Lakini Israeli wote na Yuda wakampenda Daudi; kwa kuwa alitoka na kuingia mbele yao.

17. Kisha Sauli akamwambia Daudi, Tazama, binti yangu mkubwa, Merabu, huyu nitakupa wewe ili umwoe; ila na wewe uniwie hodari wa vita, na kuvipiga vita vya BWANA. Maana Sauli alisema moyoni mwake, Mkono wangu usiwe juu yake, bali mkono wa Wafilisti na uwe juu yake.

18. Naye Daudi akamwambia Sauli, Mimi ni nani, na jamaa zangu ni akina nani, au mbari ya babangu, katika Israeli, hata mimi niwe mkwewe mfalme?

19. Lakini ikawa, wakati ule, ilipopasa Daudi apewe Merabu, binti Sauli, aliolewa na Adrieli, Mmeholathi.

20. Walakini Mikali, binti Sauli, alimpenda Daudi; watu wakamwambia Sauli, na neno hilo likampendeza.

1 Sam. 18