1 Sam. 12:5-19 Swahili Union Version (SUV)

5. Akawaambia, BWANA ni shahidi juu yenu, na masihi wake ni shahidi leo, ya kuwa hamkuona kitu mkononi mwangu. Nao wakasema, Yeye ni shahidi.

6. Samweli akawaambia watu, Ni yeye BWANA aliyewaweka Musa na Haruni, ndiye yeye aliyewatoa baba zenu kutoka nchi ya Misri.

7. Basi sasa simameni, ili niwahutubie mbele za BWANA, kwa kutaja matendo yote ya haki ya BWANA, aliyowatendea ninyi na baba zenu.

8. Yakobo alipokuwa ameingia Misri, na baba zenu walipomlilia BWANA, ndipo BWANA akawapeleka Musa na Haruni, nao wakawatoa baba zenu kutoka Misri, wakawakalisha mahali hapa.

9. Lakini wakamsahau BWANA, Mungu wao, naye akawauza na kuwatia katika mikono ya Sisera, jemadari wa jeshi la Hazori, na katika mikono ya Wafilisti, na katika mikono ya mfalme wa Moabu, nao wakapigana nao.

10. Nao wakamlilia BWANA, wakasema, Tumefanya dhambi, kwa kuwa tumemwacha BWANA, na kuwatumikia Mabaali na Maashtorethi; lakini sasa utuokoe na mikono ya adui zetu, nasi tutakutumikia wewe.

11. BWANA akawatuma Yerubaali, na Baraka, na Yeftha, na Samweli, akawaokoa ninyi na mikono ya adui zenu pande zote, nanyi mkakaa salama.

12. Hata mlipomwona Nahashi, mfalme wa wana wa Amoni, amekuja kupigana nanyi, mliniambia, Sivyo, lakini mfalme atatutawala; ingawa BWANA, Mungu wenu, ni mfalme wenu.

13. Basi sasa, mtazameni mfalme mliyemchagua na kumtaka; tazameni, BWANA ameweka mfalme juu yenu.

14. Kama mkimcha BWANA, na kumtumikia, na kuisikia sauti yake, msiiasi amri ya BWANA, tena kama ninyi, na mfalme anayewatawala, mkimfuata BWANA, Mungu wenu, vema!

15. Bali msipoisikia sauti ya BWANA, mkiiasi amri ya BWANA, ndipo mkono wa BWANA utakuwa juu yenu, kama ulivyokuwa juu ya baba zenu.

16. Na sasa simameni, mkalione jambo hili kubwa, BWANA atakalolitenda mbele ya macho yenu.

17. Leo je! Si mavuno ya ngano? Nitamwomba BWANA, kwamba apeleke ngurumo na mvua; nanyi mtajua na kuona ya kuwa uovu wenu ni mwingi sana, mlioufanya machoni pa BWANA, kwa kujitakia mfalme.

18. Basi Samweli akamwomba BWANA, naye BWANA akapeleka ngurumo na mvua siku ile; nao watu wote wakamwogopa BWANA sana, na Samweli pia.

19. Watu wote wakamwambia Samweli, Utuombee sisi watumwa wako kwa BWANA, Mungu wako, tusije tukafa; maana tumeongeza dhambi zetu zote kwa uovu huu, wa kujitakia mfalme.

1 Sam. 12