1 Sam. 12:15-25 Swahili Union Version (SUV)

15. Bali msipoisikia sauti ya BWANA, mkiiasi amri ya BWANA, ndipo mkono wa BWANA utakuwa juu yenu, kama ulivyokuwa juu ya baba zenu.

16. Na sasa simameni, mkalione jambo hili kubwa, BWANA atakalolitenda mbele ya macho yenu.

17. Leo je! Si mavuno ya ngano? Nitamwomba BWANA, kwamba apeleke ngurumo na mvua; nanyi mtajua na kuona ya kuwa uovu wenu ni mwingi sana, mlioufanya machoni pa BWANA, kwa kujitakia mfalme.

18. Basi Samweli akamwomba BWANA, naye BWANA akapeleka ngurumo na mvua siku ile; nao watu wote wakamwogopa BWANA sana, na Samweli pia.

19. Watu wote wakamwambia Samweli, Utuombee sisi watumwa wako kwa BWANA, Mungu wako, tusije tukafa; maana tumeongeza dhambi zetu zote kwa uovu huu, wa kujitakia mfalme.

20. Samweli akawaambia, Msiogope; ni kweli mmeutenda uovu huu wote; lakini msigeuke na kuacha kumfuata BWANA, bali mtumikieni BWANA kwa mioyo yenu yote.

21. Wala msigeuke upande, maana, kufuata vitu vya ubatili,

22. visivyoweza kusaidia wala kuokoa, kwa kuwa havifai kitu. Maana BWANA hatawaacha watu wake kwa ajili ya jina lake kuu; kwa kuwa imempendeza BWANA kuwafanya ninyi kuwa watu wake mwenyewe.

23. Walakini mimi, hasha! Nisimtende BWANA dhambi kwa kuacha kuwaombea ninyi; lakini nitawaelimisha katika njia iliyo njema, na kunyoka

24. Mcheni BWANA tu, mkamtumikie kwa kweli kwa mioyo yenu yote; maana, kumbukeni jinsi alivyowatendea mambo makuu.

25. Lakini kama mkiendelea kutenda mabaya, mtaangamia, ninyi na mfalme wenu pia.

1 Sam. 12