1 Nya. 29:5-19 Swahili Union Version (SUV)

5. ya dhahabu, kwa vitu vya dhahabu, na ya fedha kwa vitu vya fedha, na kwa kazi za kila namna zitakazofanywa kwa mikono ya mafundi. Ni nani basi ajitoaye kwa moyo ili ajiweke wakfu leo kwa BWANA?

6. Ndipo wakuu wa mbari za mababa, na wakuu wa kabila za Israeli, na maakida wa maelfu na wa mamia, pamoja na wasimamizi wa kazi ya mfalme, wakajitoa kwa hiari yao;

7. nao wakatoa, kwa ajili ya utumishi wa nyumba ya Mungu, dhahabu talanta elfu tano, na darkoni elfu kumi, na fedha talanta elfu kumi, na shaba talanta elfu kumi na nane, na chuma talanta elfu mia.

8. Na wale walioonekana kuwa na vito vya thamani wakavitoa vitiwe katika hazina ya nyumba ya BWANA, chini ya mkono wa Yehieli, Mgershoni.

9. Ndipo hao watu wakafurahi, kwa sababu wametoa kwa hiari yao wenyewe, kwa sababu kwa ukamilifu wa moyo, kwa hiari yao wenyewe, wamemtolea BWANA; mfalme Daudi naye akafurahi kwa furaha kuu.

10. Kwa hiyo Daudi akamhimidi BWANA, mbele ya mkutano wote; naye Daudi akasema, Uhimidiwe, Ee BWANA, Mungu wa Israeli baba yetu, milele na milele.

11. Ee BWANA, ukuu ni wako, na uweza, na utukufu, na kushinda, na enzi; maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako; ufalme ni wako, Ee BWANA, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote.

12. Utajiri na heshima hutoka kwako wewe, nawe watawala juu ya vyote; na mkononi mwako mna uweza na nguvu; tena mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote.

13. Basi sasa, Mungu wetu, twakushukuru na kulisifu jina lako tukufu.

14. Lakini mimi ni nani, na watu wangu ni nani, hata tuweze kutoa kwa hiari hivi? Kwani vitu vyote vyatoka kwako na katika vitu vyako mwenyewe tumekutolea.

15. Kwani sisi tu wageni mbele zako, na wasafiri, kama walivyokuwa baba zetu wote; ni kama kivuli siku zetu duniani, wala taraji ya kukaa hapana.

16. Ee BWANA, Mungu wetu, akiba hii yote tuliyoiweka, ili tukujengee nyumba kwa ajili ya jina lako takatifu, yatoka yote mkononi mwako, na yote ni yako wewe.

17. Nami najua, Mungu wangu, ya kuwa wewe wajaribu moyo, nawe wapendezwa na unyofu. Nami katika unyofu wa moyo wangu nimeyatoa haya yote kwa hiari yangu mwenyewe; nami sasa nimeona kwa furaha watu wako, waliopo hapa, wakikutolea kwa hiari yao.

18. Ee BWANA, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, baba zetu, ulilinde jambo hili milele katika fikira za mawazo ya mioyo ya watu wako, ukaiongoze mioyo yao kwako;

19. naye Sulemani mwanangu, umpe moyo mkamilifu, ili azishike amri zako, na shuhuda zako, na maagizo yako, akayatende hayo yote na kuijenga nyumba hii ya enzi, niliyoiwekea akiba.

1 Nya. 29