26. Maana miungu yote ya watu si kitu;Lakini BWANA ndiye aliyezifanya mbingu.
27. Heshima na adhama ziko mbele zake;Nguvu na furaha zipo mahali pake.
28. Mpeni BWANA, enyi jamaa za watu,Mpeni BWANA utukufu na nguvu.
29. Mpeni BWANA utukufu wa jina lake;Leteni sadaka, mje mbele zake;Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu;
30. Tetemekeni mbele zake, nchi yote.Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike;
31. Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie;Na waseme katika mataifa, BWANA ametamalaki;
32. Bahari na ivume na vyote viijazavyo;Mashamba na yashangilie na vyote vilivyomo;
33. Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha,Mbele za BWANA,Kwa maana anakuja aihukumu nchi.
34. Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema;Kwa maana fadhili zake ni za milele.
35. Nanyi mkaseme,Ee Mungu wa wokovu wetu, utuokoe,Utukusanye kwa kututoa katika mataifa,Tulishukuru jina lako takatifu,Tuzifanyie shangwe sifa zako.
36. Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, tangu milele hata milele. Na watu wote wakasema, Amina; wakamhimidi BWANA.
37. Basi akawaacha huko, mbele ya sanduku la agano la BWANA, Asafu na nduguze, ili watumike mbele ya sanduku daima, kila siku kama ilivyokuwa kazi yake.
38. Naye Obed-edomu, pamoja na ndugu zao, sitini na wanane; Obed-edomu na mwana wa Yeduthuni, na Hosa, wawe mabawabu;
39. na Sadoki kuhani, na nduguze makuhani, mbele ya maskani ya BWANA katika mahali pa juu palipokuwa huko Gibeoni,
40. ili kumtolea BWANA sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa daima asubuhi na jioni, naam, sawasawa na yote yaliyoandikwa katika torati ya BWANA, aliyowaamuru Israeli;
41. na pamoja nao Hemani na Yeduthuni, na wale wengine waliochaguliwa, waliotajwa majina yao, ili kumshukuru BWANA, kwa kuwa fadhili zake ni za milele;
42. na pamoja nao Hemani na Yeduthuni wenye baragumu na matoazi, kwa hao watakaovumisha sauti, na vinanda kwa ajili ya hizo nyimbo za Mungu; na hao wana wa Yeduthuni wawepo mlangoni.
43. Kisha watu wote wakaenda zao kila mtu nyumbani kwake; naye Daudi akarudi ili awabariki watu wa nyumbani mwake.