1. Wakaliingiza sanduku la Mungu, na kuliweka katikati ya hema aliyoipiga Daudi kwa ajili yake; wakatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Mungu.
2. Na Daudi alipokwisha kuitoa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani, akawabariki watu kwa jina la BWANA.
3. Kisha akawagawia kila mtu wa Israeli, waume kwa wake, kila mtu mkate wa ngano, na kipande cha nyama, na mkate wa zabibu.
4. Akawaagiza baadhi ya Walawi kwamba watumike mbele ya sanduku la BWANA, wamfanyie ukumbusho, na shukrani, na sifa, BWANA, Mungu wa Israeli;
5. Asafu mkuu wao, na wa pili wake Zekaria, na Yeieli, na Shemiramothi, na Yehieli, na Matithiya, na Eliabu, na Benaya, na Obed-edomu, na Yeieli, wenye vinanda na vinubi; naye Asafu mwenye kupiga matoazi;
6. nao makuhani Benaya na Yahazieli wenye baragumu daima, mbele ya sanduku la agano la Mungu.
7. Ndipo siku hiyo Daudi alipoagiza kwanza kumshukuru BWANA, kwa mkono wa Asafu na nduguze.
8. Mshukuruni BWANA, liitieni jina lake;Wajulisheni watu matendo yake.
9. Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi;Zitafakarini ajabu zake zote.
10. Jisifuni kwa jina lake takatifu;Na ufurahi moyo wao wamtafutao BWANA.