1 Kor. 7:9-24 Swahili Union Version (SUV)

9. Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa.

10. Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza; wala hapo si mimi, ila Bwana; mke asiachane na mumewe;

11. lakini, ikiwa ameachana naye, na akae asiolewe, au apatane na mumewe; tena mume asimwache mkewe.

12. Lakini watu wengine nawaambia mimi, wala si Bwana, ya kwamba iwapo ndugu mmoja ana mke asiyeamini, na mke huyo anakubali kukaa naye asimwache.

13. Na mwanamke, ambaye ana mume asiyeamini, na mume huyo anakubali kukaa naye, asimwache mumewe.

14. Kwa maana yule mume asiyeamini hutakaswa katika mkewe; na yule mke asiyeamini hutakaswa katika mumewe; kama isingekuwa hivyo, watoto wenu wangekuwa si safi; bali sasa ni watakatifu.

15. Lakini yule asiyeamini akiondoka, na aondoke. Hapo huyo ndugu mume au ndugu mke hafungiki. Lakini Mungu ametuita katika amani.

16. Kwa maana wajuaje, wewe mwanamke, kama utamwokoa mumeo? Au wajuaje, wewe mwanamume, kama utamwokoa mkeo?

17. Lakini kama Bwana alivyomgawia kila mtu, kama Mungu alivyomwita kila mtu, na aenende vivyo hivyo. Ndivyo ninavyoagiza katika makanisa yote.

18. Je! Mtu fulani ameitwa hali amekwisha kutahiriwa? Asijifanye kana kwamba hakutahiriwa. Mtu fulani ameitwa hali hajatahiriwa bado? Basi asitahiriwe.

19. Kutahiriwa si kitu, na kutokutahiriwa si kitu bali kuzihifadhi amri za Mungu.

20. Kila mtu na akae katika hali ile ile ambayo alikuwa nayo alipoitwa.

21. Je! Uliitwa u mtumwa? Usione ni vibaya lakini kama ukiweza kuwa na uhuru, afadhali kuutumia.

22. Kwa maana yeye aliyeitwa katika Bwana hali ya utumwa, ni huru wa Bwana. Vivyo hivyo yeye naye aliyeitwa hali ya uhuru, ni mtumwa wa Kristo.

23. Mlinunuliwa kwa thamani; msiwe watumwa wa wanadamu.

24. Ndugu zangu, kila mtu na akae mbele za Mungu katika hali iyo hiyo aliyoitwa nayo.

1 Kor. 7