1 Fal. 16:3-15 Swahili Union Version (SUV)

3. angalia, kuondoa nitawaondoa Baasha na jamaa yake; tena nitaifanya nyumba yako iwe kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati.

4. Mtu amfiaye Baasha mjini mbwa watamla; naye amfiaye mashambani ndege wa angani watamla.

5. Basi, mambo yote ya Baasha yaliyosalia, na aliyoyafanya, na nguvu zake, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?

6. Baasha akalala na babaze, akazikwa katika Tirza; naye Ela mwanawe akatawala mahali pake.

7. Tena neno la BWANA likaja kwa mkono wa nabii Yehu mwana wa Hanani juu ya Baasha, na juu ya nyumba yake, kwa sababu ya mabaya yote aliyoyatenda machoni pa BWANA, akimghadhibisha kwa kazi ya mikono yake, kwa kufanana na nyumba ya Yeroboamu, na kwa sababu aliiharibu.

8. Katika mwaka wa ishirini na sita wa Asa mfalme wa Yuda, Ela mwana wa Baasha alianza kutawala juu ya Israeli huko Tirza, akatawala miaka miwili.

9. Na mtumwa wake Zimri, jemadari wa nusu ya magari yake, akamfanyia fitina; alipokuwako Tirza akinywa hata kulewa nyumbani mwa Arsa, aliyekuwa juu ya nyumba huko Tirza;

10. Zimri akaingia akampiga, akamwua, katika mwaka wa ishirini na saba wa Asa mfalme wa Yuda, akatawala mahali pake.

11. Ikawa, alipoanza kutawala, mara alipoketi juu ya kiti chake cha enzi, akawaua nyumba yote ya Baasha; hakumwachia mwanamume ye yote, wa jamaa zake, wala wa rafiki zake.

12. Hivyo Zimri akaiharibu nyumba yote ya Baasha, sawasawa na neno la BWANA, alilolinena juu ya Baasha kwa Yehu nabii,

13. kwa sababu ya makosa yake Baasha, na makosa yote ya Ela mwanawe, waliyoyakosa, na kuwakosesha Israeli, wakimghadhibisha BWANA, Mungu wa Israeli, kwa matendo yao ya ubatili.

14. Na mambo yote ya Ela yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?

15. Katika mwaka wa ishirini na saba wa Asa mfalme wa Yuda, Zimri akatawala muda wa siku saba huko Tirza. Basi, watu walikuwa wametua maragoni kupigana na Gibethoni, ulio wa Wafilisti.

1 Fal. 16