Yoe. 2:5-20 Swahili Union Version (SUV)

5. Kama mshindo wa magari ya vita juu ya vilele vya milima, ndivyo warukavyo; kama mshindo wa miali ya moto ilapo mabua makavu, kama mashujaa waliopangwa tayari kwa vita.

6. Mbele yao watu wanahangaika; nyuso zote zimegeuka kuwa nyeupe kwa hofu.

7. Hupiga mbio kama mashujaa; huupanda ukuta kama watu wa vita; nao huendelea mbele kila mmoja katika njia zake, wala hawapotoshi safu zao.

8. Wala hapana mmoja amsukumaye mwenzake; huendelea mbele kila mmoja katika njia yake; hujifanyizia njia kwa nguvu kati ya silaha, wala hawaachi kuifuata njia yao.

9. Huurukia mji; hupiga mbio juu ya ukuta; hupanda na kuingia ndani ya nyumba; huingia madirishani kama aingiavyo mwivi.

10. Nchi inatetemeka mbele yao; mbingu zinatetemeka; jua na mwezi hutiwa giza, na nyota huacha kuangaza;

11. naye BWANA anatoa sauti yake mbele ya jeshi lake; maana matuo yake ni makubwa sana; kwa maana yeye ni hodari atekelezaye neno lake; kwa kuwa siku ya BWANA ni kuu, yenye kitisho sana; naye ni nani awezaye kuistahimili?

12. Lakini hata sasa, asema BWANA, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea;

13. rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie BWANA, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya.

14. N’nani ajuaye kwamba hatarudi na kugeuka, na kutuachia baraka nyuma yake, naam, sadaka ya unga, na sadaka ya kinywaji, kwa BWANA, Mungu wenu?

15. Pigeni tarumbeta katika Sayuni,Takaseni saumu, kusanyeni kusanyiko kuu;

16. Kusanyeni watu, litakaseni kusanyiko,Kusanyeni wazee, kusanyeni watoto,Na hao wanyonyao maziwa;Bwana arusi na atoke chumbani mwake,Na bibi arusi katika hema yake.

17. Hao makuhani, wahudumu wa BWANA, na walieKati ya patakatifu na madhabahu,Na waseme, Uwaachilie watu wako, Ee BWANA,Wala usiutoe urithi wako upate aibu,Hata mataifa watawale juu yao;Kwani waseme kati ya watu, Yuko wapi Mungu wao?

18. Hapo ndipo BWANA alipoona wivu kwa ajili ya nchi yake, akawahurumia watu wake.

19. BWANA akajibu, akawaambia watu wake; Tazameni, nitawaletea nafaka, na divai, na mafuta, nanyi mtashiba kwa vitu hivyo; wala sitawafanya tena kuwa aibu kati ya mataifa;

20. lakini jeshi lililotoka kaskazini nitaliondolea mbali nanyi, nami nitalifukuza mpaka nchi ya ukame na ukiwa; sehemu yake iliyo mbele itaingia katika bahari ya mashariki, na sehemu yake iliyo nyuma itaingia katika bahari ya magharibi; na uvundo wake utapanda juu, na harufu yake mbaya itapanda juu, kwa sababu ametenda mambo makubwa.

Yoe. 2