Yer. 51:31-50 Swahili Union Version (SUV)

31. Tarishi mmoja atapiga mbio kumlaki mwingine,Na mjumbe mmoja atapiga mbio kumlaki mwenziwe,Ili kumpasha habari mfalme wa Babeli,Ya kuwa mji wake umetwaliwa kila upande.

32. Navyo vivuko vimeshambuliwa,Nayo makangaga wameyatia moto,Nao watu wa vita wameingiwa na hofu.

33. Kwa maana BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi; Binti Babeli amekuwa kama sakafu ya kufikichia wakati wa kukanyagwa kwake; bado kitambo kidogo na wakati wa mavuno utafika kwake.

34. Nebukadreza, mfalme wa Babeli, amenila, ameniseta, amenifanya kuwa chombo kitupu; amenimeza kama joka, amelijaza tumbo lake vitu vyangu vya anasa; amenitupa

35. Udhalimu niliotendwa mimi, na uliotendwa mwili wangu, umpate Babeli; ndivyo atakavyosema yeye akaaye Sayuni; na Yerusalemu atasema, Damu yangu na iwe juu yao wakaao katika Ukaldayo.

36. Basi, BWANA asema hivi, Tazama, nitakutetea, nami nitatwaa kisasi kwa ajili yako; nami nitaikausha bahari yake, nitaifanya chemchemi yake kuwa pakavu.

37. Na Babeli utakuwa magofu, makao ya mbwa-mwitu, ajabu, na mazomeo, pasipo mtu wa kukaa huko.

38. Watanguruma pamoja kama wana-simba; watanguruma kama simba wachanga.

39. Wakiingiwa na ukali, nitawafanyizia karamu yao, nami nitawalevya, wapate kufurahi, na kulala usingizi wa milele, wasiamke tena, asema BWANA.

40. Nitawatelemsha kama wana-kondoo machinjoni, kama kondoo waume pamoja na mabeberu.

41. Jinsi Sheshaki alivyotwaliwa!Naye sifa ya dunia yote alivyoshambuliwa!Jinsi Babeli alivyokuwa ukiwaKatikati ya mataifa!

42. Bahari imefika juu ya Babeli,Umefunikwa kwa wingi wa mawimbi yake.

43. Miji yake imekuwa maganjo;Nchi ya ukame, na jangwa;Nchi asimokaa mtu ye yote,Wala hapiti mwanadamu huko.

44. Nami nitafanya hukumu juu ya Beli katika Babeli, nami nitavitoa katika kinywa chake alivyovimeza; wala mataifa hawatamwendea tena; naam, ukuta wa Babeli utaanguka.

45. Enyi watu wangu; tokeni katikati yake, mkajiokoe nafsi zenu na hasira kali ya BWANA, kila mmoja wenu.

46. Wala isizimie mioyo yenu, wala msiiogope habari itakayosikiwa katika nchi; maana habari itakuja mwaka mmoja, na baadaye mwaka wa pili habari itakuja, na udhalimu katika nchi, mwenye kutawala akishindana na mwenye kutawala.

47. Basi angalia, siku zitakuja, ambazo katika siku hizo, nitafanya hukumu juu ya sanamu za Babeli, na nchi yake yote itatahayarika; na watu wake wote waliouawa wataanguka katikati yake.

48. Ndipo mbingu, na nchi, na vitu vyote vilivyomo, vitaimba kwa furaha juu ya Babeli; kwa maana watu waangamizao watamjilia kutoka kaskazini, asema BWANA.

49. Kama vile Babeli alivyowaangusha watu wa Israeli waliouawa, ndivyo watakavyoanguka katika Babeli watu wa nchi yake nzima waliouawa.

50. Ninyi mliojiepusha na upanga,Enendeni zenu, msisimame;Mkumbukeni BWANA tokea mbali,Na Yerusalemu ukatiwe mioyoni mwenu.

Yer. 51