Yer. 46:8-22 Swahili Union Version (SUV)

8. Misri anajiinua kama mto Nile,Na maji yake yanajirusha kama mito;Asema, Nitajiinua, nitaifunikiza nchi;Nitauharibu mji na hao wakaao ndani yake.

9. Haya! Pandeni, enyi farasi;Jihimizeni, enyi magari ya vita;Mashujaa nao na watoke njeKushi na Puti, watumiao ngao;Nao Waludi, washikao uta na kuupeta.

10. Maana hiyo ni siku ya Bwana, BWANA wa majeshi,Siku ya kisasi, ili ajilipize kisasi juu ya adui zake;Nao upanga utakula na kushiba,Utakunywa damu yao hata kukinai;Maana Bwana, BWANA wa majeshi, ana sadaka yakeKatika nchi ya kaskazini karibu na mto Frati.

11. Panda uende Gileadi, ukatwae zeri, Ee binti, bikira wa Misri; unatumia dawa nyingi bure tu; hupati kupona kamwe.

12. Mataifa wamesikia habari za aibu yako, nayo dunia imejaa kilio chako; maana shujaa amejikwaa juu ya shujaa mwenzake, wameanguka wote wawili pamoja.

13. Neno hili ndilo ambalo BWANA alimwambia Yeremia, nabii, kueleza jinsi Nebukadreza, mfalme wa Babeli, atakavyokuja na kuipiga nchi ya Misri.

14. Tangazeni habari hii katika Misri, mkaihubiri katika Migdoli, na kuihubiri katika Nofu, na Tahpanesi; semeni, Simama, ujifanye tayari kwa maana upanga umekula pande zako zote.

15. Mbona mashujaa wako wamechukuliwa mbali? Hawakusimama kwa sababu BWANA aliwafukuza.

16. Aliwakwaza wengi, naam, wakaangukiana wao kwa wao; wakasema, Haya! Na tuondoke, tukarudi kwa watu wetu wenyewe, hata nchi tuliyozaliwa, tuukimbie upanga unaotuonea.

17. Wakalia huko, Farao, mfalme wa Misri, ni kishindo tu; muhula alioandikiwa ameuacha upite.

18. Kama mimi niishivyo, asema Mfalme, ambaye jina lake ni BWANA wa majeshi, hakika yake, kama Tabori katika milima, na kama Karmeli karibu na bahari, ndivyo atakavyokuja.

19. Ee binti ukaaye katika Misri,Ujiweke tayari kwenda zako hali ya kufungwa;Kwa maana Nofu utakuwa ukiwa,Utateketezwa, usikaliwe na watu.

20. Misri ni mtamba mzuri sana, lakini uharibifu umekuja,Umekuja utokao pande za kaskazini.

21. Na watu wake waliojiwa, walio kati yake,Ni kama ndama waliowanda malishoni;Maana wao nao wamerudi nyuma,Wamekimbia wote pamoja, wasisimame;Maana siku ya msiba wao imewafikilia,Wakati wa kujiliwa kwao.

22. Sauti yake ni kama nyoka, wajapo kwa nguvu,Watamjia na mashoka, kama wachanja kuni.

Yer. 46