Yer. 36:3-13 Swahili Union Version (SUV)

3. Huenda nyumba ya Yuda watasikia mabaya yote niliyokusudia kuwatenda; wapate kurudi, kila mtu akaiache njia yake mbaya; nami nikawasamehe uovu wao na dhambi yao.

4. Kisha Yeremia akamwita Baruku, mwana wa Neria; naye Baruku akaandika katika gombo la chuo maneno yote ya BWANA, yaliyotoka kinywani mwa Yeremia, ambayo BWANA amemwambia.

5. Yeremia akamwagiza Baruku, ya kwamba, Mimi nimefungwa, siwezi kuingia katika nyumba ya BWANA.

6. Basi, enenda wewe, ukasome katika gombo la chuo, ambacho umeandika ndani yake, maneno ya BWANA yaliyotoka kinywani mwangu, ukiyasoma katika masikio ya watu, ndani ya nyumba ya BWANA, siku ya kufunga; pia utayasoma masikioni mwa watu wote wa Yuda, watokao katika miji yao.

7. Labda wataomba dua zao mbele za BWANA, na kurudi, kila mtu akiiacha njia yake mbaya; kwa maana hasira na ghadhabu ni kuu sana, alizotamka BWANA juu ya watu hawa.

8. Basi, Baruku, mwana wa Neria, akafanya sawasawa na hayo yote, ambayo Yeremia, nabii, amemwagiza, akisoma katika chuo hicho, maneno ya BWANA, ndani ya nyumba ya BWANA.

9. Basi, ikawa katika mwaka wa tano wa Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, katika mwezi wa kenda, watu wote waliokuwa katika Yerusalemu, na watu wote waliokuja Yerusalemu kutoka miji yote ya Yuda, wakapiga mbiu ya kufunga mbele za BWANA.

10. Basi, wakati huo Baruku akayasoma maneno ya Yeremia katika nyumba ya BWANA, katika chumba cha Gemaria, mwana wa Shafani, mwandishi, katika ua wa juu, mahali pa kuingilia kwa lango jipya la nyumba ya BWANA, akiyasoma katika masikio ya watu wote.

11. Basi, Mikaya, mwana wa Gemaria, mwana wa Shafani, aliposikia maneno yote ya BWANA yaliyokuwa katika chuo hicho,

12. akashuka, akaingia katika nyumba ya mfalme, katika chumba cha mwandishi, na, tazama, wakuu wote wameketi humo, nao ni hawa, Elishama, mwandishi, na Delaya, mwana wa Shemaya, na Elnathani, mwana wa Akbori, na Gemaria, mwana wa Shafani, na Sedekia, mwana wa Hanania, na wakuu wote.

13. Naye Mikaya akawaeleza maneno yote aliyoyasikia, hapo Baruku alipokuwa akikisoma kitabu masikioni mwa watu.

Yer. 36