Yer. 36:1-7 Swahili Union Version (SUV)

1. Ikawa katika mwaka wa nne wa Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili likamjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, kusema,

2. Twaa gombo la chuo, ukaandike ndani yake maneno yote niliyokuambia juu ya Israeli, na juu ya Yuda, na juu ya mataifa yote, tangu siku ile niliponena nawe, tangu siku za Yosia, hata siku hii ya leo.

3. Huenda nyumba ya Yuda watasikia mabaya yote niliyokusudia kuwatenda; wapate kurudi, kila mtu akaiache njia yake mbaya; nami nikawasamehe uovu wao na dhambi yao.

4. Kisha Yeremia akamwita Baruku, mwana wa Neria; naye Baruku akaandika katika gombo la chuo maneno yote ya BWANA, yaliyotoka kinywani mwa Yeremia, ambayo BWANA amemwambia.

5. Yeremia akamwagiza Baruku, ya kwamba, Mimi nimefungwa, siwezi kuingia katika nyumba ya BWANA.

6. Basi, enenda wewe, ukasome katika gombo la chuo, ambacho umeandika ndani yake, maneno ya BWANA yaliyotoka kinywani mwangu, ukiyasoma katika masikio ya watu, ndani ya nyumba ya BWANA, siku ya kufunga; pia utayasoma masikioni mwa watu wote wa Yuda, watokao katika miji yao.

7. Labda wataomba dua zao mbele za BWANA, na kurudi, kila mtu akiiacha njia yake mbaya; kwa maana hasira na ghadhabu ni kuu sana, alizotamka BWANA juu ya watu hawa.

Yer. 36