Yer. 31:9-18 Swahili Union Version (SUV)

9. Watakuja kwa kulia, na kwa maombi nitawaongoza; nitawaendesha penye mito ya maji, katika njia iliyonyoka; katika njia hiyo hawatajikwaa; maana mimi ni baba wa Israeli, na Efraimu ni mzaliwa wa kwanza wangu.

10. Lisikieni neno la BWANA, enyi mataifa, litangazeni visiwani mbali; mkaseme, Aliyemtawanya Israeli atamkusanya, na kumlinda, kama mchungaji alindavyo kundi lake.

11. Kwa maana BWANA amemweka huru Yakobo, amemkomboa mkononi mwake aliyekuwa hodari kuliko yeye.

12. Nao watakuja, na kuimba katika mlima Sayuni, wataukimbilia wema wa BWANA, nafaka, na divai, na mafuta, na wachanga wa kondoo na wa ng’ombe; na roho zao zitakuwa kama bustani iliyotiwa maji; wala hawatahuzunika tena kabisa.

13. Ndipo bikira atafurahi katika kucheza, na vijana na wazee pamoja; maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha, nami nitawafariji, na kuwafurahisha waache huzuni zao.

14. Nami nitaishibisha roho ya makuhani kwa unono, na watu wangu watashiba kwa wema wangu, asema BWANA

15. BWANA asema hivi,Sauti imesikiwa Rama,kilio, na maombolezo mengi,Raheli akiwalilia watoto wake;asikubali kufarijiwa kwa watoto wake, kwa kuwa hawako,

16. BWANA asema hivi,Zuia sauti yako, usilie,na macho yako yasitoke machozi;Maana kazi yako itapata thawabu,nao watakuja tena toka nchi ya adui;Ndivyo asemavyo BWANA.

17. Tena liko tumaini kwa siku zako za mwisho, asema BWANA; na watoto wako watarejea hata mpaka wao wenyewe.

18. Hakika nimemsikia Efraimu, akijililia hivi, Umeniadhibu, nami nikaadhibika, kama ndama asiyeizoelea nira; unigeuze, nami nitageuzwa; kwa maana wewe u BWANA, Mungu wangu.

Yer. 31