17. Tena liko tumaini kwa siku zako za mwisho, asema BWANA; na watoto wako watarejea hata mpaka wao wenyewe.
18. Hakika nimemsikia Efraimu, akijililia hivi, Umeniadhibu, nami nikaadhibika, kama ndama asiyeizoelea nira; unigeuze, nami nitageuzwa; kwa maana wewe u BWANA, Mungu wangu.
19. Hakika baada ya kugeuzwa kwangu, nalitubu; na baada ya kufundishwa kwangu, nalijipiga pajani; nalitahayarika, naam, nalifadhaika, kwa sababu naliichukua aibu ya ujana wangu.
20. Je! Efraimu siye mwanangu mpendwa? Je! Siye mtoto apendezaye? Maana kila nisemapo neno juu yake, ningali nikimkumbuka sana; kwa sababu hiyo moyo wangu unataabika kwa ajili yake; bila shaka nitamrehemu, asema BWANA.
21. Jiwekee alama za njia; jifanyie miti ya kukuongoza; uuelekeze moyo wako kwenye njia kuu, njia ile ile uliyoiendea; rudi tena, Ee bikira wa Israeli, irudie hii miji yako.
22. Hata lini utatanga-tanga, Ee binti mwenye kuasi? Kwa maana BWANA ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanamume.