Yer. 17:8-18 Swahili Union Version (SUV)

8. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji,Uenezao mizizi yake karibu na mto;Hautaona hofu wakati wa hari ujapo,Bali jani lake litakuwa bichi;Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua,Wala hautaacha kuzaa matunda.

9. Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?

10. Mimi, BWANA, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.

11. Kama kware akusanyaye makinda asiyoyazaa, ndivyo alivyo mtu ajipatiaye mali, wala si kwa haki, katikati ya siku zake zitaachana naye, na mwisho wake atakuwa mpumbavu.

12. Kiti cha enzi, cha utukufu, kilichowekwa juu tangu mwanzo, ndicho mahali patakatifu petu.

13. Ee BWANA, tumaini la Israeli, wote wakuachao watatahayarika. Wao watakaojitenga nami wataandikwa katika mchanga, kwa sababu wamemwacha BWANA, kisima cha maji yaliyo hai.

14. Uniponye, Ee BWANA, nami nitaponyeka; uniokoe, nami nitaokoka; kwa maana wewe ndiwe uliye sifa zangu.

15. Tazama, wao waniambia, Neno la BWANA liko wapi? Na lije, basi.

16. Mimi hapa sikufanya haraka kuacha kuwa mchungaji nyuma yako; wala sikuitamani siku ya maradhi ya kufisha; wewe unajua; yaliyotoka midomoni mwangu yalikuwa mbele za uso wako.

17. Usiwe sababu ya hofu kuu kwangu mimi; wewe ndiwe uliye kimbilio langu siku ya uovu.

18. Na waaibike watu wanaoniudhi, lakini nisiaibike mimi; na waone hofu kuu, lakini mimi nisione hofu kuu; ulete juu yao siku ya uovu; uwaangamize maangamizo maradufu.

Yer. 17