7. Ijapokuwa maovu yetu yanatushuhudia, lakini utende wewe kwa ajili ya jina lako, Ee BWANA, maana kurudi nyuma kwetu ni kwingi; tumekutenda dhambi.
8. Wewe uliye tumaini la Israeli, wewe uliye Mwokozi wake wakati wa taabu, kwa nini wewe umekuwa kama mtu akaaye katika nchi, hali ya mgeni, na kama mtu mwenye kusafiri, ageukaye upande ili kukaa usiku mmoja tu?
9. Kwa nini wewe umekuwa kama mtu aliyesituka, kama shujaa asiyeweza kuokoa? Lakini wewe, BWANA, u katikati yetu, nasi tunaitwa kwa jina lako; usituache.
10. BWANA awaambia watu hawa hivi, Hivyo ndivyo walivyopenda kutanga-tanga; hawakuizuia miguu yao; basi, BWANA hawakubali; sasa ataukumbuka uovu wao, atawapatiliza dhambi zao.
11. Naye BWANA akaniambia, Usiwaombee watu hawa wapate heri.
12. Wafungapo, mimi sitasikia kilio chao; na watoapo sadaka za kuteketezwa na sadaka ya unga, sitazitakabali; bali nitawaangamiza kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni.
13. Ndipo nikasema, Aa, Bwana, MUNGU! Tazama, manabii huwaambia, Hamtauona upanga, wala hamtakuwa na njaa; bali nitawapa amani iliyo thabiti mahali hapa.
14. Ndipo BWANA akaniambia, Hao manabii wanatabiri uongo kwa jina langu mimi; mimi sikuwatuma, wala sikuwaamuru, wala sikusema nao; wanawapeni unabii wa maono ya uongo, na uaguzi, na neno la ubatili, na hadaa ya mioyo yao.
15. Basi, kwa hiyo BWANA asema hivi, Kwa habari za manabii wanaotabiri kwa jina langu, wala mimi sikuwatuma, lakini husema, Upanga na njaa havitaingia katika nchi hii; Kwa upanga na njaa manabii hao wataangamizwa.