Yer. 14:10-20 Swahili Union Version (SUV)

10. BWANA awaambia watu hawa hivi, Hivyo ndivyo walivyopenda kutanga-tanga; hawakuizuia miguu yao; basi, BWANA hawakubali; sasa ataukumbuka uovu wao, atawapatiliza dhambi zao.

11. Naye BWANA akaniambia, Usiwaombee watu hawa wapate heri.

12. Wafungapo, mimi sitasikia kilio chao; na watoapo sadaka za kuteketezwa na sadaka ya unga, sitazitakabali; bali nitawaangamiza kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni.

13. Ndipo nikasema, Aa, Bwana, MUNGU! Tazama, manabii huwaambia, Hamtauona upanga, wala hamtakuwa na njaa; bali nitawapa amani iliyo thabiti mahali hapa.

14. Ndipo BWANA akaniambia, Hao manabii wanatabiri uongo kwa jina langu mimi; mimi sikuwatuma, wala sikuwaamuru, wala sikusema nao; wanawapeni unabii wa maono ya uongo, na uaguzi, na neno la ubatili, na hadaa ya mioyo yao.

15. Basi, kwa hiyo BWANA asema hivi, Kwa habari za manabii wanaotabiri kwa jina langu, wala mimi sikuwatuma, lakini husema, Upanga na njaa havitaingia katika nchi hii; Kwa upanga na njaa manabii hao wataangamizwa.

16. Na watu hao, waliopewa unabii na wao, watatupwa nje katika njia kuu za Yerusalemu kwa sababu ya upanga na njaa; wala hawatakuwa na mtu wa kuwazika, wao na wake zao, na wana wao, na binti zao; maana nitamwaga uovu wao wenyewe juu yao.

17. Nawe utawaambia neno hili, Macho yangu na yatiririke machozi, usiku na mchana, wala yasikome; kwa maana bikira, binti ya watu wangu, amevunjika mavunjiko makuu, kwa jeraha isiyoponyeka.

18. Nikitoka kwenda shambani, tazama, wako huko waliouawa kwa upanga! Na nikiingia mjini, tazama, wamo humo wanaougua kwa sababu ya njaa! Maana nabii na kuhani, wote wawili, huenda huko na huko katika nchi, wala hawana maarifa.

19. Je! Umemkataa Yuda kabisa? Roho yako imeichukia Sayuni? Mbona umetupiga, tusiwe na dawa ya kutuponya? Tulitazamia amani, lakini hayakuja mema yo yote, tulitazamia wakati wa kupona, na tazama, kufadhaika tu!

20. Ee BWANA, tunakiri uovu wetu, na ubaya wa baba zetu; maana tumekutenda dhambi.

Yer. 14