1. Wewe u mwenye haki, Ee BWANA, nitetapo nawe, lakini nitasema nawe katika habari ya haki. Mbona njia ya wabaya inasitawi? Mbona wote watendao hila wanakaa salama?
2. Umewapanda, naam, wametia mizizi, wanakua, naam, wanazaa matunda; katika vinywa vyao u karibu, bali katika mioyo yao u mbali.
3. Lakini wewe, BWANA, wanijua; umeniona, umeujaribu moyo wangu, jinsi unavyokuelekea; uwakokote kama kondoo waendao kuchinjwa, ukawaweke tayari kwa siku ya kuchinjwa.
4. Hata lini itaomboleza nchi, na kukauka majani ya nchi yote? Kwa ajili ya mabaya yao wakaao ndani yake, wanyama wameangamia na ndege pia; kwa sababu walisema, Hatauona mwisho wetu.
5. Ikiwa umepiga mbio pamoja na hao waendao kwa miguu, nao wamekuchosha, basi wawezaje kushindana na farasi? Na ujapokuwa katika nchi ya amani u salama, lakini utafanyaje hapo katika kiburi cha Yordani?
6. Kwa maana hata ndugu zako, na nyumba ya baba yako, wamekutenda mambo ya hila; naam, wamepiga kelele nyuma yako; usiwasadiki, wajapokuambia maneno mazuri.