4. Ukimpeleka ndugu yetu pamoja nasi, tutashuka na kukununulia chakula.
5. Ila usipompeleka, hatushuki, maana mtu yule alituambia, Hamtaniona uso wangu, ndugu yenu asipokuwa pamoja nanyi.
6. Israeli akasema, Mbona mmenitendea vibaya hata mkamwarifu mtu yule ya kwamba mna ndugu mwingine?
7. Wakasema, Mtu yule alituhoji sana habari zetu na za jamaa yetu, akisema, Baba yenu angali hai? Mnaye ndugu mwingine? Nasi tukamjibu sawasawa na maswali hayo. Je! Tuliweza kujua ya kwamba atasema, Shukeni pamoja na ndugu yenu?
8. Yuda akamwambia Israeli babaye, Mpeleke kijana pamoja nami, tuondoke, tuende zetu, ili tupate kuishi, wala tusife, sisi na wewe na watoto wetu.
9. Mimi nitakuwa mdhamini wake, umtake mkononi mwangu. Nisipomleta tena kwako, na kumweka mbele yako, nitakuwa mwenye hatia mbele yako daima;
10. maana kama hatungalikawia, hakika tungaliisha kurudi mara ya pili.
11. Israeli, baba yao, akawaambia, Kama ndivyo, fanyeni hivi; twaeni tunu za nchi katika vyombo vyenu, mkamchukulie mtu huyo zawadi, zeri kidogo, na asali kidogo, ubani, na manemane, na jozi, na lozi.
12. Mkatwae fedha maradufu mikononi mwenu, na fedha zile zilizorudishwa kinywani mwa magunia yenu zirudisheni mikononi mwenu; labda zilisahauliwa.
13. Mtwaeni na ndugu yenu, mwondoke na kurudi kwa mtu yule.
14. Mungu Mwenyezi na awape rehema usoni pa mtu yule ili awafungulie ndugu yenu huyo mwingine, na Benyamini. Nami nikifiwa na watoto wangu, nimefiwa.
15. Basi hao watu wakatwaa zawadi ile, wakatwaa na fedha maradufu mikononi mwao, na Benyamini; wakaondoka, wakashuka mpaka Misri, wakasimama mbele ya Yusufu.
16. Naye Yusufu alipomwona Benyamini pamoja nao, akamwambia msimamizi wa nyumba yake, Uwalete watu hawa nyumbani, ukachinje na kuandalia, maana watu hawa watakula pamoja nami adhuhuri.
17. Yule mtu akafanya kama Yusufu alivyomwambia Naye akawaleta watu hao nyumbani mwa Yusufu.
18. Lakini watu hao wakaogopa kwa sababu wameletwa nyumbani mwa Yusufu, wakasema, Kwa sababu ya fedha zile zilizorudishwa katika magunia yetu mara ya kwanza tumeletwa humu; apate kutushitaki, na kutuangukia, atutwae sisi kuwa watumwa, na punda zetu.