26. Navyo ndivyo walivyofanyiwa. Wakaweka nafaka yao juu ya punda zao, wakatoka huko.
27. Mmoja wao alipofungua gunia lake ili ampe punda wake chakula katika nyumba ya wageni, aliiona fedha yake; kumbe! Iko kinywani mwa gunia lake.
28. Akawaambia nduguze, Fedha yangu imerudishwa, angalia, imo humo guniani mwangu. Mioyo yao ikazimia, wakageukiana wakitetemeka, wakasema, N’nini hii Mungu aliyotutendea?
29. Wakaja kwa Yakobo, baba yao, katika nchi ya Kanaani, wakampasha habari za yote yaliyowapata, wakisema,
30. Mtu yule aliye bwana wa nchi alisema nasi kwa maneno makali, akatufanya tu wapelelezi wa nchi.
31. Tukamwambia, Tu watu wa kweli sisi, wala si wapelelezi.
32. Sisi tu ndugu kumi na wawili, wana wa baba yetu. Mmoja hayuko, na mdogo wetu yuko pamoja na baba yetu leo katika nchi ya Kanaani.
33. Yule mtu, bwana wa nchi, akatuambia, Kwa njia hii nitawajua kama ninyi ni watu wa kweli; ndugu yenu mmoja mwacheni huku kwangu, kachukueni nafaka kwa njaa ya nyumba zenu, mwende zenu.
34. Mkaniletee ndugu yenu mdogo; ndipo nitakapojua kama ninyi si wapelelezi, bali ni watu wa kweli; basi nitawarudishia ndugu yenu, nanyi mtafanya biashara katika nchi hii.
35. Ikawa walipomimina magunia yao, kumbe! Bahasha ya fedha ya kila mtu imo katika gunia lake. Nao walipoziona bahasha za fedha zao, wao na baba yao waliogopa.
36. Yakobo baba yao akawaambia, Mmeniondolea watoto wangu; Yusufu hayuko, wala Simeoni hayuko, na Benyamini mnataka kumchukua naye; mambo hayo yote yamenipata mimi.