37. Neno hilo likawa jema machoni pa Farao, na machoni pa watumwa wake wote.
38. Farao akawaambia watumwa wake, Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya Mungu ndani yake?
39. Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe.
40. Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.
41. Farao akamwambia Yusufu, Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misri.
42. Farao akavua pete yake ya muhuri mkononi mwake, akaitia mkononi mwa Yusufu; akamvika mavazi ya kitani nzuri, na kumtia mkufu wa dhahabu shingoni mwake.
43. Akampandisha katika gari lake la pili alilokuwa nalo. Na watu wakapiga kelele mbele yake, Pigeni magoti. Hivyo akamweka juu ya nchi yote ya Misri.
44. Farao akamwambia Yusufu, Mimi ni Farao, na bila amri yako, mtu asiinue mkono wala mguu katika nchi yote ya Misri.
45. Farao akamwita Yusufu, Safenath-panea; akamwoza Asenathi, binti Potifera, kuhani wa Oni, kuwa mkewe Yusufu akaenda huko na huko katika nchi yote ya Misri.
46. Naye Yusufu alikuwa mwenye miaka thelathini, aliposimama mbele ya Farao, mfalme wa Misri. Yusufu akatoka mbele ya uso wa Farao, akapita katika nchi yote ya Misri.
47. Ikawa katika miaka ile saba ya shibe, nchi ikazaa kwa wingi.