2. Hata baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani, peke yao; akageuka sura yake mbele yao;
3. mavazi yake yakimeta-meta, meupe mno, jinsi asivyoweza dobi duniani kuyafanya meupe.
4. Wakatokewa na Eliya pamoja na Musa, nao walikuwa wakizungumza na Yesu.
5. Petro akajibu, akamwambia Yesu, Rabi, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu, kimoja chako wewe, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya.
6. Maana, hakujua la kunena, kwa kuwa waliingiwa na hofu nyingi.
7. Kisha likatokea wingu, likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye.
8. Mara hiyo walipotazama huku na huku, hawakuona mtu pamoja nao ila Yesu peke yake.
9. Na walipokuwa wakishuka mlimani aliwakataza wasimweleze mtu waliyoyaona, hata Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka katika wafu.